Mabomu ya arthini yategwa Mali
Wapiganaji wa kiisilamu
kaskazini mwa Mali wametega mabomu ya arthini mjini Gao baada ya
kuudhibiti wiki jana.Wakaazi wa eneo hilo wamesema wapiganaji hao
wametega mabomu hayo ili kuzuia mashambulizi ya kundi hasimu la Tuareg.
Makundi yote yalishirikiana katika harakati za
kudhibiti kaskazini mwa Mali baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi hapo
mwezi Aprili.Wakati huo huo Ufaransa imesema katu haitakubalia magaidi
kuweka ngome zao nchini Mali.
Waziri Mkuu wa Ufaransa Jean-Marc
Ayrault ametaja kundi la Al Qaeda Afrika Kaskazini{AQIM} kama tisho
kubwa kwa usalama katika kanda kaskazini mwa Afrika na pia kwa Ufaransa.
Matamshi ya Waziri Mkuu yanajiri wakati kundi
linaloshirikiana na mtandao wa Al Qaeda Ansar Dine limeharibu misikiti
ya kale mjini Timbuktu kwa tuhuma za kujengwa kinyume na Sharia ya
Kiisilamu.
Mwendesha mashataka mkuu katika Mahakama ya
Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita Fatou Bensouda, amelaani uharibifu huo na
kuutaja kama uhalifu wa kivita. Wakaazi katika mji wa Gao wamesema
wapiganaji wa kundi la Kiisilamu wametishia maisha yao kwa kuyatega
mabomu hayo. Maduka mengi yamefungwa na watu wamesalia manyumbani.
Wapiganaji wa Tuareg ambao wanadaiwa kutaka
kuushambulia mji huo wanataka kujitenga na Mali na kuunda eneo huru bila
kuzingatia sera za dini. Aidha kundi hili limelaani uharibifu
uliotekelezwa na kundi hasimu la Ansar Dine mjini Timbuktu.Msukosuko huu
unaoendelea kaskazini mwa Mali umepelekea watu 300,000 kukimbia makaazi
yao.
No comments:
Post a Comment