Marekani yataja makundi hatari Afrika
Makundi matatu ya kigaidi Barani
Afrika yameanza kushirikiana katika harakati zao. Hii ni kwa mujibu wa
Mkuu wa jeshi la Marekani anayesimamia shughuli za usalama kanda ya
Afrika. Jenerali Cater Ham amesema kundi la Al Qaeda Afrika Kaskazini
limekuwa likiwasaidia wanachama wa Boko Haram nchini Nigeria na mabomu.
Akizungumza mjini Washington afisa huyo amesema
waasi wanaodhibiti kaskazini mwa Mali wameendelea kutumia eneo hilo
kuendesha harakati zao ikiwemo kupanga njama za kutekeleza
mashambulio.Jenerali Ham ni kamanda wa kitengo cha idara ya ulinzi ya
marekani kinachofuatilia masuala ya usalama barani Afrika{Africom} na
makao makuu yako Ujerumani.
Kitengo hiki kinaimrisha harakati
zozote za kijeshi Afrika ikiwemo mashambulio ya kutumia ndege bila
rubani dhidi ya wapiganaji wa Kisomali wa Al shabaab.
Tayari kuna wanajeshi 100 wa Marekani
wanaosaidia kumsaka kiongozi wa waasi Uganda Joseph Kony ambao
wanasimamiwa na kitengo cha Jenerali Ham.
Afisa huyo ametaja makundi hatari zaidi ikiwa ni pamoja na kundi la Al Qaeda Afrika Kaskazini{AQIM}, Boko Haram na Al-Shabab.
Ameongeza tisho kubwa ni kwamba makundi haya yameanza kushirikiana katika kufanikisha harakati zao.
Mapema mwaka huu nchi ya Mali ilishuhudia
mapinduzi ya kijeshi na kufuatiwa na kudhibitiwa kwa eneo nzima la
Kaskazini na makundi yanayotetea kujitenga ya Tuareg na wapiganaji wa
kiisilamu.
No comments:
Post a Comment