Thursday, September 20, 2012

Chelsea yashindwa kuifunga Juventus


Chelsea
Mabingwa watetezi Chelsea katika uwanja wa nyumbani walishindwa kuibwaga Juventus
Mabingwa watetezi wa klabu bingwa barani Ulaya, Chelsea ya Uingereza, wakicheza katika uwanja wa nyumbani wa Stamford Bridge, walishindwa kuifunga Juventus ya Italia katika pambano la Jumatano usiku.
Nyota wa Chelsea alikuwa ni mchezaji Oscar kutoka Brazil, ambaye alifanikiwa kutumbukiza magoli mawili wavuni katika kipindi cha kwanza; dakika ya 31 na 33.
Bao la pili liliingia kupitia mkwaju wa mbali, na ambalo lilimuacha kipa wa Juventus, Gianluigi Buffon akiwa amezubaa.
Oscar alisajiliwa na Chelsea hivi majuzi.
Hata hivyo Juventus, mabingwa wa Italia, na ambao hawakushindwa katika mechi 42 za Serie A huko nyumbani, walijikakamua na hatimaye kusawazisha na kujinyakulia pointi moja.
Arturo Vidal aliwafungia bao kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika, na baadaye mchezaji wa zamu, Fabio Quagliarella, zikiwa zimesalia dakika tisa mechi kumalizika, alithibitisha Juventus ilikuwa na nia ya kuondoka na angalau pointi moja.
Kati ya mechi nane za Jumatano, Manchester United pia ilikuwa uwanjani kupambana na Galatasaray, na vijana wa Sir Alex Ferguson wakichezea nyumbani, mechi ya kundi G, walipata ushindi wa bao 1-0.
Michael Carrick aliandikisha bao hilo mapema, dakika ya 7.
Klabu hiyo ya Uturuki itadhaniwa na wengi kwamba ilinyimwa nafasi ya kusawazisha, kwa mwamuzi kuwapa penalti, baada ya Nemanja Vidic kumchezea vibaya Umut Bulup.

No comments:

Post a Comment

SHARE

TOA MAONI YAKO KUHUSU POST HII

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...