Ligi kuu ya soka ya Tanzania
Bara iliendelea tena september 19 ambapo timu zote 14 zimeshuka katika
viwanja tofauti kutafuta pointi tatu muhimu ambapo Dar es salaam
mabingwa watetezi wa ligi hiyo wekundu wa Msimbazi Simba wameendeleza
wimbi la ushindi baada ya kuichapa JKT Ruvu 2 kwa 0.
Simba imefanikiwa kupata
ushindi huo ikiwa pungufu baada ya mshambuliaji wake wa kimataifa kutoka
Uganda Emmanuel Okwii kuonyeshwa kadi nyekundu katika kipindi cha
kwanza.
Magoli ya Simba yalifungwa na
viungo Amri Kiemba na Haruna Moshi ‘Boban’ na kwa matokeo hayo, Simba
inaendelea kuongoza ligi kwa kufikisha pointi sita baada ya awali
kuifunga African Lyon 3-0.
Kocha wa JKT Ruvu Charles
Kilinda amesema wamepoteza mchezo huo kutokana na kufanya makosa ambayo
yamesababisha mabao mepesi kwa wapinzani wao lakini kocha wa Simba
Milovan Cirkovic amesema haukuwa ushindi mwepesi hasa ukizingatia timu
yake ilicheza pungufu kwa muda mrefu na amemlaumu mwamuzi wa mchezo huo
kwa kusema kadi nyekundu aliyomuonyesha Emmanuel Okwii haikuwa sahihi
kwani alistahili kadi ya njano.
Wakati Simba wakiwa Dar es
salaam wapinzani wao Dar es salaam Young Africans walikuwa na kibarua
kingine kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar ambapo
Yanga walichapwa 3-0 hivyo Yanga waliziacha pointi tatu muhimu mbele ya
Mtibwa.
Kwenye mechi iliyochezwa Mwanza
Toto Afrika walilazimishwa sare nyingine katika uwanja wa nyumbani
baada ya kutoka sare ya 2 kwa 2 dhidi ya Azam FC kwenye uwanja wa CCM
Kirumba.
Tanzania Prisons na Coastal
Union walitoka 1-1, Kagera Sugar na JKT Oljoro hawakufungana, kwenye
game iliyochezwa Mbagala Chamazi African Lyon iliishinda Polisi Morogoro
1-0, Ruvu Shooting Stars wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani Pwani
wameifunga JKT Mgambo 2 kwa 1.
Dar es salaam Young Africans
kwa mara ya kwanza wataonekana jijini Dar es salaam katika ligi kuu ya
msimu huu kwa kuvaana na JKT Ruvu kwenye uwanja wa taifa wakati Azam fc
watajitupa kwenye uwanja wao wa Azam Complex Chamazi kuwakaribisha
Mtibwa Sugar kutoka Morogoro.
No comments:
Post a Comment