Alama za Freemason.
WAISLAMU duniani kote wapo kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani lakini gumzo lililotawala katika misikiti mingi jijini Dar ni juu ya dini ya kishetani ya Freemason ambapo waumini wengi wamevutika kutaka kuijua kwa undani.
Hilo limekuja kufuatia mawaidha ambayo yamekuwa yakitolewa na mwanaharakati wa dini ya Kiislamu, Ustadhi Rajab Milanzi ambaye ndani ya kipindi hiki amekuwa akipita misikitini na kufichua mazito kuhusiana na Freemason.
Akiwa kwenye nyumba hizo za ibada hivi karibuni, ustaadhi huyo amekuwa akielezea asili ya dini hiyo, jinsi inavyofanya kazi, malengo pamoja na madhara yake katika Uislamu.
Ni gumzo misikiti
Mawaidha ya Ustadhi Milanzi (pichani) yamezua gumzo katika misikiti mbalimbali jijini Dar ambapo kila waumini wamalizapo kuswali, wamekuwa wakikusanyika katika vikundi huku mada kubwa ikiwa ni Freemason.
Risasi Mchanganyiko lilifanikiwa kukutana na ustadhi huyo katika Msikiti wa Mwenge Bamaga jijini Dar ambapo mbali na kuwataka Waislamu kujiweka mbali na dini hiyo ya shetani, amesisitiza kuhakikisha anafikisha ujumbe huo kwa kila Muislamu.
Anasema: “Chama cha shetani ni ukafiri na kwenye chama hiki cha Freemason Mungu wao ni Ibilisi. Malengo yao makubwa ni kuitawala dunia kwa kitu kinachoitwa ‘The New World Order’. Waislamu hawatakiwi kuingia huko.”
Kufuatia mawaidha hayo, mijadala juu ya dini hiyo imeshika kasi huku uchunguzi ukionesha kuwa, licha ya madhara yanayotajwa bado kuna wanaoshawishika kujiunga kwa lengo la kusaka mafanikio.
Mashehe wacharuka
Kitendo cha baadhi ya waumini kuendelea kuwa na imani kuwa kufanikiwa kwao kunaweza kuja kwa kujiunga na dini hiyo, kimewafanya baadhi ya mashehe kucharuka na kueleza kuwa, endapo Muislamu yeyote atashawishika kujiunga ‘automatikale’ atakuwa amejitoa kwenye Uislamu.
Akiongea na gazeti hili, shehe Idrisa Juma wa msikiti mmoja uliopo Mbagala jijini Dar alisema, amesikitishwa na baadhi ya Waislamu wanaoishabikia dini hiyo bila kujua kuwa wanamchukiza Mwenyezi Mungu.
“Ni kweli mjadala juu ya Freemason ni mkubwa na hapa msikitini kwangu haipiti siku bila kukuta watu wakiijadili kwa mapana na marefu.
“Nadhani imetokana na mawaidha anayotoa ustadhi Milanzi na CD yake aliyota kuhusu Freemason, naamini wengi watajifunza na mimi nitahakikisha nafikisha ujumbe kwa waumini wangu ili wajiweke mbali na dini hiyo,” alisema Shehe huyo.
Shehe mwingine wa msikiti mmoja uliopo Magomeni ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema, ameshangazwa na jinsi Waislamu wengi walivyovutika na taarifa za Freemason hasa kipindi hiki huku baadhi wakihaha kutaka kujiunga.
“Unajua kipindi kama hiki cha mwezi mtukufu Waislamu wengi hutumia muda mwingi kujadili mambo mbalimbali yanayohusu Uislamu lakini safari hii kila kona utakumbana na mijadala juu ya Freemason, kazi tuliyonayo ni kuhakikisha watu wetu hawaingii huko,” alisema shehe huyo.
Baadhi waitamani Freemason
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, licha ya viongozi hao wa dini ya Kiislamu kuwaelimisha waumini wao juu ya madhara ya kujiunga na dini hiyo, wapo ambao wanahisi wanabaniwa ili wasifanikiwe kimaisha.
Muumini aliyejitambulisha kwa jina la Hussein Salim wa Sinza jijini Dar alisema: “Mimi nawashangaa hawa viongozi wetu wanaotuogopesha tusijiunge na Freemason.
“Ninavyojua Freemason ni dini kama dini nyingine na tunaona watu ambao wanatajwa kuwa wanachama maisha yao ni safi, sasa kuna ubaya gani na mimi kutafuta mafanikio kwa njia hiyo? Sijajua tu namna ya kujiunga lakini natamani hata leo…”
Katika siku za hivi karibuni Freemason imekuwa gumzo kila pembe ya nchi huku viongozi wa dini mbalimbali wakitahadharisha waumini wao kutojiunga nayo kwa madai kuwa, inakwenda kinyume na maandiko ya Mwenyezi Mungu.
No comments:
Post a Comment