Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinalaani uamuzi wa Serikali
inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulifungia kwa muda
usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kwa kutumia mwanya wa sheria mbovu ya
magazeti inayokwenda kinyume na haki za binadamu na utawala bora.
CHADEMA
kinaitaka Serikali kulifungulia gazeti hilo haraka iwekanavyo na
kimewasiliana na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA
kuchukua hatua za kibunge kuisimamia Serikali kurekebisha udhaifu huo
ikiwa inaheshimu uhuru wa habari na inazingatia maslahi ya taifa.
CHADEMA
kinatafsiri hatua hiyo ya Serikali ya kufungia gazeti la MwanaHalisi
kuwa ni sawa na kufungia uhuru wa kusambaza habari, uhuru wa kupokea
habari na uhuru wa kutoa maoni, hivyo tunatoa mwito kwa wananchi na
wadau wote wa habari kuungana pamoja kupinga hatua hiyo, na CHADEMA
kitaeleza hatua za ziada za kuchukuliwa iwapo Serikali haitasikiliza
kauli za wadau wa habari juu ya suala hili.
CHADEMA
kinatambua kuwa uamuzi wa Serikali kufungia gazeti hilo kwa mara
nyingine tena ni kwenda kinyume na haki za binadamu, kinyume na utawala
bora na ni kikwazo kwa demokrasia na maendeleo nchini.
CHADEMA
kinapinga hatua ya Serikali ambayo viongozi na watendaji wake wakiwa
wametajwa kama watuhumiwa katika habari zilizoandikwa na gazeti hilo
imetumia mamlaka haramu ya Waziri mwenye dhamana ya sekta ya habari
kugeuka mlalamikaji, mwendesha mashtaka na mfungaji huku ikipuuza
taasisi za kusimamia uwajibikaji na haki.
CHADEMA
ilitarajia badala ya kulifungia gazeti la MwanaHalisi ingewezesha
kufanyika kwa uchunguzi huru kufuatia habari za kiuchunguzi
zilizoandikwa na gazeti hilo juu ya watendaji na watumishi wa Serikali
kuhusishwa na jaribio la mauji ya Dr Ulimboka Steven, kupanga njama za
mauji ya viongozi wa CHADEMA na matukio mengine ambayo yenyewe ndiyo
yenye mwelekeo wa kufanya wananchi wapoteze imani na vyombo vya dola
hali ambayo inaweza kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini.
CHADEMA
kinalinganisha uamuzi huo wa Serikali uliotangazwa tarehe 30 Julai 2012
na Msajili wa Magazeti chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo kuwa ni sawa kujichukulia sheria mikononi kwa kuwa Serikali
yenye kuheshimu misingi ya asili ya haki ingezingatia kwamba ikiwa
chombo chochote cha habari kimedaiwa kuvunja sheria ama kukiuka maadili
dhidi ya Serikali, viongozi wake ama watu binafsi mashtaka au malalamiko
yangepelekwa kwa taasisi zinazohusika mathalani Baraza la Habari (MCT)
au mahakama.
CHADEMA kinafahamu kuwa Serikali imeamua
kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi,
kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu Na. (25) (i);
hata hivyo uamuzi huo ni kinyume cha misingi ya asili ya utawala wa
sheria.
CHADEMA kinaelewa kwamba zipo sheria nyingine
katika nchi yetu ambazo Serikali ingeweza kuzitumia kushughulikia madai
iliyoyatoa kuwa Gazeti la Mwanahalisi limeandika habari na makala za
uchochezi, uhasama na uzushi kupitia mahakama lakini imeamua kwa
makusudi kuendelea kutumia sheria mbaya isiyokuwa na uhalali wa kihaki
(illegitimate).
CHADEMA kinakumbusha kuwa kwamba Sheria
hiyo ni kati ya Sheria zilizotajwa na Tume ya kukusanya maoni juu ya
mfumo wa vyama vingi (Tume ya Nyalali) kuwa ni sheria mbaya miaka 20
iliyopita kuwa na Sheria mbaya na Serikali imekuwa ikikwepa kutunga
sheria mpya pamoja na wadau wa habari kuandaa miswada ya sheria ya
huduma za vyombo vya habari na uhuru wa taarifa kwa nyakati mbalimbali.
CHADEMA
kinatoa mwito kwa wananchi na taasisi zote za kitaifa na kimataifa
kufuatilia kwa karibu tukio hili la kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi
na matukio mengine ya hivi karibuni kuhusu asasi za kiraia, makundi
mbalimbali katika jamii ikiwemo madaktari na vyama vya siasa hususan
CHADEMA yenye kuashiria kwamba Serikali inayoongozwa na CCM imeanza
mkakati wa kuficha ukweli na kudhibiti mabadiliko kwa kutumia sheria
kandamizi, vyombo vya dola na njia nyingine haramu.
Hivyo,
ieleweke kwamba hatua hii dhidi ya Gazeti la MwanaHalisi ni mwanzo tu
wa hatua zingine zaidi dhidi ya magazeti mengine na taasisi nyingine
hali ambayo inahitaji wananchi na wadau wote kuunganisha nguvu za pamoja
katika kuchukua hatua za haraka kuinusuru nchi na mwelekeo huo.
Imetolewa tarehe 30 Julai 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment