Akimsomea mashtaka hayo mbele
ya hakimu mkazi wa mahakama ya Kisutu Faisal Kahamba, Mwendesha mashtaka
wakili mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka amesema kosa la kwanza Dr
Mkopi anashitakiwa kwa kutotii amri halali ya mahakama kuu kitengo cha
kazi iliyomtaka atangaze kusitisha mgomo wa madaktari.
Wakili Kweka amesema kosa hilo
ni kinyume cha kanuni ya adhabu namba 124 ambapo kosa la pili
linalomkabili Dr Mkopi ni kuhamasisha mgomo wa Madaktari kinyume na
kanuni na adhabu ya kifungu cha 390 na kifungu cha 35.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo
Dr Mkopi aliyakana yote ambapo mawakili wake wanne wanaomtetea
wakiongozwa na Kikondo Maulid wameomba mteja wao apatiwe dhamana ambapo
hakimu mkazi Faisal Kahamba amesema dhamana ipo wazi na kutaja masharti
ya dhamana hiyo ambayo yalipingwa na mawakili wa upande wa utetezi.
Masharti ya dhamana yaliyotajwa
yalikua ni wadhamini wawili waajiriwa wa serikali au taasisi
zinazotambulika kisheria wakiwa na vitambulisho vyao na hati ya mali
isiyopungua thamani ya shilingi laki tano ambapo mawakili wa upande wa
mashitaka walitaka masharti ya kukabidhi hati ya kusafiria na kuzuiwa
kusafiri nje ya Dar es salaam ndio yaingizwe kwenye masharti ya dhamana.
Hali hiyo ya mvutano wa
kisheria ilimlazimu hakimu huyo jana Mahakamani kuomba muda wa dakika
kumi ili apitie sheria husika na baada ya hapo mahakama iliamua
kumuachia Dr Mkopi kwa masharti yaliyotajwa awali ambapo hakimu
alitangaza kwamba kama kuna mtu hajaridhia dhamana hiyo anaweza kukata
rufaa mahakama kuu hivyo akaiahirisha kesi hiyo mpaka mwezi wa nane
tarehe 6 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment