YANGA jana imeanza vibaya
michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati baada ya kufungwa 2-0
na Atletico ya Burundi Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mabao mawili ya Olivier
Ndikumana katika dakika ya 81 na 90+3, yalitosha kuipa Atletico FC
ushindi wa 2-0 dhidi ya mabingwa hao watetezi, huku Yanga ikiwa imecheza
ovyo pamoja na kuzidiwa katika kila idara- angalau baada ya kufungwa
bao la kwanza walijaribu kushambulia kwa mipira ya pembeni lakini
walipopigwa la pili katika dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya
dakika 90 kupita ‘walitepeta kabisa’.
Yanga ilikuwa ikicheza mechi
ya pili chini ya kocha mpya Mbelgiji Tom Saintfiet baada ya mechi ya
awali ya kirafiki dhidi ya JKT Ruvu ambayo timu hiyo ilishinda 2-,
Falsafa ya Tom anayeingia katika wiki ya pili tangu atue Jangwani ni
kucheza soka ya utulivu, zaidi wakipaki basi- wakati umaarufu wa Yanga
kwa muda mrefu ni soka yao ya kasi na pasi ndefu, zaidi wakitumia
mashambulizi ya kutokea pembeni na ndio maana mawinga wengi bora na
maarufu nchini walicheza Yanga, hii ni tangu enzi za akina Awadh Gessan,
Leonard Chitete, Abubakar Salum ‘Sure Boy’, Sanifu Lazaro ‘Tingisha’,
Edibilly Lunyamila, Ephraim Makoye, Mrisho Ngassa na wengineo.
Yanga wapo kwenye kipindi cha
mpito kuelekea katika mabadiliko ya mfumo wa uchezaji ambao ukifanikiwa
utakuwa bora zaidi na wenye tija.
No comments:
Post a Comment