Wizara ya Afya ya Uganda
imetangaza kuwa ugonjwa wa Ebola umeibuka tena, na wakuu wa afya
wanasema hadi sasa umeuwa watu 13, na watu 7 wengine wameambukizwa
virusi vya ugonjwa huo.
Maafisa wanasema ugonjwa huo ulijitokeza mwezi wa Juni, na wanajitahidi kuudhibiti usitapakae.
Wakuu wanasema mtu wa kwanza kufa kwa ugonjwa
huo ni mwanamke mja mzito, ambaye alitanguliwa na mtoto wake mchanga, na
yeye mwenyewe punde akamfuata.
Wanasema watu wengi waliokufa walikuwa jamaa wa karibu, ambao waliambukizwa mazikoni au wakati wanawauguza wagonjwa.
Wagonjwa wengi ni kutoka wilaya ya Kibaale, jimbo la magharibi mwa Uganda.
Wizara ya Afya inasema imechukua hatua za
dharura katika eneo hilo, na imewasihi wenyeji wa huko waepuke
mikusanyiko mikubwa ya watu, hasa mazishi.
Tangu mwaka 2,000 ugonjwa wa Ebola umeshajitokeza mara tatu nchini Uganda.
Na wizara ya Afya inamchunguza mgonjwa mmoja
ambaye wanafikiri anauguwa Ebola, katika hospitali ya rufaa ya Mulago,
mjini Kampala.
Dr Anthony Mbonye, mkuu wa idara ya afya ya
jamii, anasema wakuu wanajitahidi kuhakikisha kuwa ugonjwa hautatapakaa
katika hospitali hiyo.
No comments:
Post a Comment