BBB

advertisement

tangaza sherehe

ADVERTISEMENT

Tuesday, July 3, 2012

CHAMA CHA WANYWA POMBE CHAANZISHWA TANZANIA

 
Leon Bahati wa Mwananchi
KILA mwaka Serikali imekuwa ikiongeza kodi kwenye vinywaji, hususan pombe ili kukidhi  bajeti ya mapato na matumizi yake. Hali hiyo husababisha bei ya pombe kupanda karibu kila mwaka na kuwaongezea mzigo wanywaji kwa kulazimika kuzama zaidi kwenye mifuko yao ili kugharimia kinywaji hicho.Kwa miaka yote hiyo wanywaji wamekuwa wakilia kimoyomoyo bila ya  kuwa na mahali pa kupaza sauti zao, hali inayoifanya Serikali ione kinywaji ni mahali kukimbilia kupata fedha.

Kulingana na taarifa za viwanda vya bia, bei ya kinywaji hicho huenda ikapanda kwa karibu asilimia 25, kuanzia mwezi huu, jambo ambalo limewafanya wanywaji kusema; “Hapana! Haiwezekani.”
Kwa sababu hiyo, wanywaji tayari wameunda jukwaa lao la kupaza sauti zao na tayari wameweka mikakakati ya kudai haki zao.Chombo hicho wamekipa jina “Chama cha Wanywa Pombe kwa Staha Tanzania (TRBDA)” na tayari kimesajiliwa na sasa kipo katika harakati za mikakati ya kukabiliana na Serikali.

“Sisi tunachotaka ni bei ya bia kushuka au kubakia palepale (Sh1,700). Hili ni suala nyeti na hatari kuliko watu wanavyolifikiria sasa,” anasema Rais wa TRBDA, Gasisi Mahuti.
Anaongeza; “Chama kimesajiliwa Mei 22 mwaka huu, hivyo tuna nguvu ya kisheria kufanya kazi na kutetea maslahi ya wanachama wetu.
“Tunaona kero kila mwaka, kila Bajeti ya Serikali wanakuja na mikakati ya kuongeza kodi kwenye pombe.”
Mahuti anasema kwa miaka mingi mzigo huo wa ongezoko la bei ya bia ambayo ndiyo inayotumiwa na watu wengi, imekuwa ikiongezeka, lakini safari hii, hali ni mbaya zaidi.
Mzigo huo kwa wanywaji anasema umechangiwa na mambo mawili makubwa ambayo ni kuongezeka kwa gharama za maisha na kiwango kikubwa cha kodi kwa mwaka huu wa fedha 2012/13 ulioanza leo.
“Hiyo bei itasababisha wanywaji wengi kuhama kwenye kinywaji salama na kwenda kwenye kinywaji hatarishi na haramu,” analalamika Mahuti.
Anavitaja vinywaji hatarishi kuwa ni baadhi ya pombe za kienyeji ambazo ni hatari kwa afya kwa sababu nyingi zinaandaliwa kwenye mazingira machafu na hakuna udhibiti. Pombe haramu anaitaja kuwa ni gongo.
Madhara ya kupandishwa bei ya pombe, anasema siyo hayo tu bali yapo ya kuathiri uchumi na maenedeleo ya watu.
“Nenda baa utaona. Siku hizi wanywaji wengi hawakai pamoja kila mmoja akiingia baa anaagiza bia yake tofauti na hapo awali mtu anazungusha ‘raundi’.
“Hili ni tatizo maana watu wengi sasa ‘hawa-socialize’. Hawakai pamoja baa kubadilishana mawazo, kupeana mbinu za maisha. Hii ni hatari,” analalamika Mahuti.
Vita na Serikali
Mahuta anasema athari za kupanda kwa bei ya bia ni nyingi na wanatarajia kuziwasilisha serikalini kutaka zipunguzwe.
Kuhusu namna watakavyowasilisha taarifa hizo, Mahuti anasema kwa kuanza watawasiliana na ofisi ya Waziri wa Fedha na Uchumi na hata likishindikana watabisha hodi ofisi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Pamoja na malalamiko hayo, anasema wamekusudia kuishawishi Serikali kubuni vyanzo vingine vya fedha ambavyo imekuwa ikishindwa kuvitumia kutokana na uzembe wa watendaji wake.
Baadhi ya sekta nchini zinapopeleka madai yake serikalini hugoma ili kutoa shinikizo.

Kuhusu wana mpango wa kugoma endapo serikali itakaidi kushusha kodi.

Kiiongozi huyo anakiri kuwa wanywaji wakigoma Serikali inaweza ikatikisika kwa sababu wanachangia pato kubwa serikalini.“Lakini sisi hatutaki kufikia huko (kugoma) au kuandamana. Sisi tunaenda kuzungumza tu hatuna haja ya kufanya fujo.

“Sisi wanywa pombe kwa staha tunatazamia busara zaidi zitatumika kuliko kulazimishana na kusababisha madhara,” anasema.Nimemuuliza, iwapo busara zitashindikana watachukua hatua gani, anasema: “Kama nilivyokuambia awali wanywa pombe walikuwa hawana jukwaa la kusemea. Sasa wanalo.

“Tunaamini kwamba Serikali ilikuwa inaongeza kodi kwa kutofahamu madhara yake ama kwa kutokuwa na vyanzo vingine. Sisi tunaenda kuwaambia madhara yake na tunaenda kuwaeleza njia nyingine za mapato. Suala la kugoma, kuandamana; halipo.”

Anasema kwa miaka mingi wanywaji ndio wamekuwa wakichangia pato la Serikali na kufanikisha utaji wa huduma mbalimbali kwa jamii kama vile elimu, afya na maji.

Ingawa wanywaji wamekuwa wakichangia hayo yote, anasema wao si wote wenye fedha sana bali wengi wao ni watu wa kipato cha kawaida.

“Mtu haindi kunywa pombe kwa sababu ana pesa nyingi. La, hasha! Ni sehemu tu ya kubadilishana mawazo na kupata maarifa. Hii ni njia ya kupashana habari,” anasema.

Majuku mengine TRBDA
Mahuti anasema jukumu la kuanzishwa kwa TRBDA siyo tu kutetea maslahi ya wateja katika suala la bei tu bali mikakati mingene ya kiafya, kijamii na kielimu.

Anasema Septemba Mosi mwaka huu kwa mara ya kwanza hapa nchini chama hicho kitaadhimisha tamasha kubwa la maadhimisho ya siku ya wanywa pombe duniani.

Anasema siku hiyo imekuwa ikisheherekewa duniani, lakini hapa nchini imekuwa haijulikani kwa sababu hakuna chombo cha uhamasishaji wa maadhimsiho.
Kwenye tamasha hilo, anasema wataeleza majukumu ya chama hicho na hata haki za wanywaji ambazo zinatambuliwa kisheria duniani.Kuwepo kwa chama hicho hapa nchini, anasema kutawezesha wanywaji kupata ushauri wa namna nzuri ya kunywa, kupimwa afya na kupewa ushauri wale ambao watagundulika kuwa na matatizo.

“Yapo magonjwa mengi ambayo huwapata watu wote kama vile presha (maradhi ya moyo) na kisukari. Watapimwa bure na ushauri bure,” anasema Mahuti.

Nimemuuliza iwapo magonjwa hayo yanasababishwa na pombe, yeye anajibu: “Hapana. Hata wasiokunywa waweza kuwa nayo. Lakini wagonjwa wa namna hii wanapaswa kushauriwa juu ya unywaji wa pombe.”

Faida nyingine kwa wanachama, anasema ni kutoa ushauri juu ya wale wanaokunywa pombe kupindukia, wanaofanya vitendo visivyofaa wanapokunywa na wale wasiotunza familia zao kutokana na ulevi.
Kwa sababu hiyo, Mahuti anasema chama pia kitapokea malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali, wakiwepo wanawake, baba ambao wanaona familia zinaathiriwa kutokana na mmoja wa wazazi kuendekeza ulevi.

“Sisi hatupendi kuona wanywaji wanasababisha kero kwenye familia. Ushauri utatolewa bure,” anasema na akifafanua: “Cha ajabu ni kwamba wengi wa Watanzania hawajui umuhimu wa kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu maisha.

Anasema katika nchi zilizoendelea ushauri nasaha wa kitaalamu kuhusu afya na maisha ni jambo la msingi hivyo mfumo huo wanataka kuuleta nchini kwa chama kugharimia wataalamu.

Wanachama ni wepi?
Mahuti anasema TRDBA kimeanzishwa na kundi dogo la watu, yeye akiwa miongoni na wala hakina mpango wa kuandikisha wanachama.Ila, anasema wanywaji wote nchini watakuwa ni wanachama wake na watahudumiwa pasipo ubaguzi wowote.Anakiri kuwa chama hicho kimepata waungaji mkono wengi wakiwepo wakurugenzi, mameneja na watendaji wakuu Serikalini na taasisi binafsi.

Hata hivyo, anasema chama hicho kinatarajia kuwa na wadau wakuu ambao ni wale wanaomiliki baa kubwa, wauzaji wa jumla, kumbi za starehe na viwanda vya pombe.

No comments:

Post a Comment

SHARE

TOA MAONI YAKO KUHUSU POST HII

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...