Katika hali ya kufurahisha waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango, wamekerwa na tabia ya wabunge wanaokwenda kwenye majimbo ya wenzao na kuanza kuwashambulia wabunge wa majimbo hayo.
Waziri Mkuu Pinda na Kilango, walionyesha hofu hiyo bungeni jana wakati wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Chanzo cha hofu hiyo kilionekana wazi baada ya Kilango kumuuliza
swali Waziri Mkuu, akitaka kujua Serikali inatoa kauli gani dhidi ya
wabunge wanaokwenda kwenye majimbo ya wenzao na kuanza kuwashambulia kwa
maneno.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa sisi wanasiasa hasa tulioko humu
bungeni tunao uwezo wa kuijenga nchi na pia tunao uwezo wa kuibomoa
nchi, napenda kujua usahihi wa hii tabia ya hivi karibuni iliyoanza
kujitokeza.
“Hivi karibuni kuna tabia imeanza kujitokeza ambayo mimi tangu
niingie humu bungeni sijawahi kuishuhudia, ambapo wabunge wanaingia
kwenye majimbo ya wenzao na kuanza kutoa maneno ya kuwasema vibaya
wabunge wenzao.
“Tabia hii ni mbaya kwa sababu inaweza kuhatarisha amani, sasa
Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujua kauli ya Serikali ni ipi juu ya
tabia hii,” alihoji Kilango.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Pinda alisema wanasiasa waliokomaa
kisiasa hawana muda wa kujadili mtu mmoja mmoja, bali wale ambao
hawajakomaa hujadili mtu mmoja mmoja.
“Naomba nitoe maelezo kidogo juu ya hali hii, ambayo nakubaliana nayo
kwamba ziko dalili za namna hiyo, kwani hata mimi yamewahi kunipata
jimboni kwangu.
“Siasa za kusemana zinategemeana na ukomavu wa kisiasa, kwani
mwanasiasa anayekwenda kwenye jimbo la mtu na kuanza kumsema mwenzake
badala ya kunadi sera za chama chake huyo hajakomaa kisiasa.
“Mwanasiasa aliyekomaa hujadili sera za chama na kuangalia ni mahali
gani panahitaji kurekebishwa, kwa hiyo hii tabia siyo nzuri.
“Kwa hiyo, rai yangu kwa wanasiasa wote ni kwamba, chonde chonde acheni siasa za aina hii,” alisema Waziri Mkuu Pinda.
No comments:
Post a Comment