Uganda inakaribisha kikosi cha Marekani
Uganda imekaribisha tangazo la
Rais Obama kuwa ametuma wanajeshi 100 wa Marekani kusaidia majeshi ya
eneo hilo kuwasaka wapiganaji wa LRA.
Msemaji
wa jeshi la Uganda, Luteni Kanali Felix Kulagye aliiambia BBC, kwamba
wanajeshi wa Marekani, watazidisha uwezo wao wa kuwapata LRA.
Kaimu Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje, Henry
Okello Oryem, alisema wamekuwa wakihitaji msaada huo kwa muda mrefu, na
wamekuwa wakiomba msaada wa kimataifa kwa miaka kadha.
LRA imekuwa ikipigana kwa miongo miwili nchini Uganda na nchi za jirani, na imeuwa maelfu ya watu.
Kiongozi wa LRA, Joseph Kony anasakwa na Mahakama ya Jinai ya Kimaiatifa, ICC.
Akitangaza hatua hiyo, Rais Obama alisema maovu yaliyotendwa na LRA ni tishio kubwa kwa usalama wa eneo hilo.
Baada ya zaidi ya miongo miwili ya muaji, kunajisi wanawake, na ubakaji, alisema wakati umefika kukifyeka kikundi hicho.
Kikosi hicho cha Marekani kitayasaidia majeshi
ya Uganda na nchi jirani katika kile kilichoelezewa kuwa, kumuondoa
kiongozi kiongozi wa LRA, Joseph Kony, vitani.
Kikosi hicho kitatumia vyombo vya teknolojia ya
kisasa kabisa, kusaidia katika kile kinachoelezewa na wadadisi, kuwa
sera ya ama kumkamata au kumuuwa Joseph Kony.
Lakini kikosi cha Marekani hakitashiriki katika mapambano ya vita, ila wakilazimika kujihami.
Kikosi hicho kimetumwa baada ya sheria
kupitishwa karibuni Marekani, inayoruhusu kusaidia kuwapokonya silaha
LRA, na kumfikisha kiongozi wake mbele ya mahakama.
Inavodhaniwa ni kuwa endapo Joseph Kony akikamatwa, basi na kikundi cha LRA kitasambaratika.
No comments:
Post a Comment