BBB

advertisement

tangaza sherehe

ADVERTISEMENT

Tuesday, June 26, 2012

Polisi wavurumishiwa mawe na wananchi kwa udhalilishaji


Mkono wa Daniel Madole uliojeruhiwa.


BAADHI ya askari Polisi wa Mkoa wa Kipoli wa Temeke jijini Dar es Salaam, wamenusurika kupigwa mawe baada ya kuvurumishiwa mawe na wananchi wenye hasira kutokana na udhalilishaji waliokuwa wakimfanyia raia aliyejulikana kwa jina la Daniel Madole (45).
Tukio hilo lilitokea Mei 31, mwaka huu Yombo Dovya wakati askari mmoja aliyejulikana kwa jina la Andrerajusi Ngosoma maarufu kwa jina la Tyson wa Kituo cha Polisi Chang’ombe Dar, kumpiga kwa fimbo na kumburuza chini kisha kumrusha kichura Madole huku akiwa amefungwa pingu mikono yote kwa nyuma .
Akizungumza na mwandishi wetu, mmoja wa wananchi hao ambao ni majirani wa Madole alisema kuwa, kutokana na udhalilishaji huo uliokuwa unafanywa hadharani walishindwa kuvumilia na kuamua kukabiliana na askari hao kwa kuwatupia mawe japokuwa waliyakwepa na kufanikiwa kumchukua mtuhumiwa.
“Kilichotushangaza ni kwamba licha ya askari wengine kumuomba Tyson asiendelee kumuadhibu Madole, alipingana nao, akaendelea kumpiga ,” alisema mwananchi mmoja ambaye jina lake tunalihifadhi.
Mwananchi huyo aliongeza kuwa baada ya kuona Madole anaendelea kuadhibiwa, waliwauliza askari sababu za kumpa kipigo kikali mtuhumiwa ndipo mmoja wao aliwafahamisha kuwa alituhumiwa kujipatia fedha shilingi 120,000 kwa njia ya udanganyifu.
Shuhuda huyo alisema baada ya kuelezwa kosa analodaiwa kulifanya mtuhumiwa huyo na kipigo kikali alichokuwa akipewa na askari hao waliokuwa na silaha za moto, walisikitika sana.
Afisa Mtendaji wa Serikali ya Mtaa wa Dovya, David Ouma alipohojiwa na gazeti hili alikiri kupokea taarifa hizo na kusema polisi walikosea kumdhalilisha mtuhumiwa huyo.
“Polisi hao wamevunja haki za binadamu kwani kama ni kesi ya madai hata mimi ningeimaliza kuliko kutumia nguvu nyingi kama walivyofanya,” alisema Ouma.
Mwandishi hakuishia hapo alimfuata Madole hadi Kituo cha Polisi Chang’ombe ambapo aliambiwa kwamba mtumiwa alipelekwa Hospitalini ya Dar Group kufuatia hali yake kuwa mbaya baada ya kupewa dhamana.
Alipopatikana alikiri kudhalilishwa na Tyson na kudai:
“Siku ya tukio polisi hao walifika kwangu saa 11 alfajiri na kukutana na mke wangu ambaye walimuuliza kama nilikuwepo ndani, alipowaambia nilikuwepo waligonga mlango nilipofungua Tyson alinifunga pingu na kuanza kunishambulia.
“Nilipomuuliza kosa langu alisema kwamba mimi ni tapeli nimechukua fedha kiasi cha shilingi 120,000 kutoka kwa mwanamke mmoja aliyetaka vyumba vya kupanga katika nyumba yangu, nilipelekwa polisi lakini nikaachiwa baadaye kwa dhamana nikiwa nimeumizwa mkono na sehemu kadhaa mwilini,” alisema.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, David Misiime (pichani) alipoulizwa juu ya tukio hilo alisema halijui na kuahidi kulifuatilia ili haki itendeke.

No comments:

Post a Comment

SHARE

TOA MAONI YAKO KUHUSU POST HII

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...