MUHIMBILI WASIWASI MTUPU
Baadhi ya wagonjwa wakisubiri huduma katika hospitali ya taifa Muhimbili.
WASIWASI mkubwa umewajaa wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam baada ya madaktari kusisitiza kuwa mgomo wao upo pale pale.
Wagonjwa mbalimbali waliolazwa katika hospitali hiyo waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa mgomo huo ulikuwa uanze rasmi Juni 23, mwaka huu, lakini haukuanza.
Hata hivyo, wagonjwa hao walidai kuwa huduma haziko katika kiwango kinachotakiwa.
Mwandishi wetu juzi Jumapili alipambana na askari walinzi ambao hawakuwa tayari kuona waandishi wakiingia wodini kuzungumza na wagonjwa.
Alibahatika kuzungumza na mgonjwa mmoja kutoka mkoani Morogoro, Kijiji cha Peko Misegese kwa sharti la kutotajwa jina ambapo alisema ana wasiwasi kutokana na tishio la mgomo wa madaktari.
Kwa upande wao manesi hospitalini hapo walisema kuwa si kweli kuwa matatizo ya nyongeza ya mishahara ndiyo chanzo pekee cha mgomo huo.
Mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina alisema kuwa kiutaratibu inatakiwa wodi moja wauguzi wasiopungua wanne lakini cha ajabu usiku mzima wanakuwa wawili tu na malipo yao kwa usiku huo ni shilingi 10,000/. Jitihada za kupata msemaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Amaniel Eligalasha ili kuzungumzia hali hiyo ziligonga mwamba kutokana na simu yake ya kiganjani kutokuwa hewani.
Mwandishi wetu alitembelea wodi mbalimbali ndani ya Kitengo cha Mifupa na Mishipa ya Fahamu, Moi na kujionea manesi wakiendelea na utoaji huduma kama kawaida hali ambayo ilitia faraja hasa kwa wagonjwa.
Msememaji wa Moi, Almas Jumaa alisema kitengo chake kipo kwa ajili ya dharura na kama kuna mgonjwa yupo wodini hawezi kuachwa kuhudumiwa.
No comments:
Post a Comment