Mlipuko wauwa mtu mmoja Mombasa
Mtu mmoja ameuwawa katika mlipuko uliotokea katika baa moja iliyoko viungani mwa mji wa Mombasa nchini Kenya.
Polisi wamesema zaidi ya watu wanane wamejeruhiwa kufuatia shambulio hilo lililotokea saa nne, Jumapili usiku.
Shambulio
hilo limejiri siku moja baada ya ubalozi wa Marekani nchini Kenya
kuonya kuwa ''kulikuwa na tisho la kutokea shambulio la kigaidi'' katika
eneo hilo.
Mapema wiki hii, maafisa wa polisi wa Kenya
waliwakamata raia wawili wa Iran waliotuhumiwa kuhusika na mtandao wa
kigaidi unaopanga kutekeleza mashambulizi mjini Mombasa.
Siku ya Jumamosi, polisi katika mji mkuu Nairobi, walisema kuwa walipata vifaa vinavyo shukiwa kutumika katika kutengeneza bomu.
aliyehusika hajakamatwa bado
Mkuu wa polisi wa mkoa wa pwani, Aggrey Adoli,
hata hivyo amesema hawezi kuhusisha moja kwa moja shambulio hilo la
Mombasa na ilani iliyotolewa na Marekani.
''Taarifa tulizopata ni kwamba kifaa hicho
ambacho tunashuku ni gruneti, kilirushwa na mtu mmoja aliyekuwa
akiburudika kwenye baa hiyo. Hatukuweza kumnasa mtu huyo lakini
tunaendelea na uchunguzi,'' Adoli aliambia kipindi cha Amka na BBC.
Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo amesema kuwa ,
wakati mlipuko huo ulipotokea, baa hiyo ilikuwa na wateja wengi
waliokuwa wakitizama mechi ya robo fainali kati ya Uingereza na Italia,
katika michuano ya kombe la taifa bingwa bara Ulaya.
Ufaransa pia ilitoa tahadhari
Mbali na Marekani, ubalozi wa Ufaransa mjini
Nairobi pia umeonya raia wake '' kuwa waangalifu'' wakiwa katika mji huo
wa Mombasa.
Marekani iliwatahadharisha raia wake kutozuru Mombasa hadi Julai mosi.
Mwezi Mei, mtu mmoja aliuwawa wakati kilipuzi kiliporushwa ndani ya mkahawa mmoja mjini humo.
Kumekuwa na msururu wa mashambulizi ya gurunedi
tangu Kenya ilipopelekwa wanajeshi wake nchini Somalia kuwasaka
wapiganaji wa kundi la kigaidi la Al- Shabab, mwezi Oktoba mwaka jana.
No comments:
Post a Comment