BBB

advertisement

tangaza sherehe

ADVERTISEMENT

Tuesday, June 26, 2012

Kama sh. trilioni 1.7 zinapotea kila mwaka serikalini, basi tumekwisha!

Spika wa Bunge Anna Makinda.
NIANZE makala haya kwa kumshukuru Mungu ambaye ametuwezesha kukutana tena katika safu hii, hakika ametupendelea wewe na mimi, hatuna cha kumpa isipokuwa kumtukuza daima kwa neema ya kuishi anayotujalia bila upendeleo.
Wengi tumesikia kuwa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2012/13 imesomwa bungeni na kupitishwa lakini kamati ya viongozi wa dini nao wameibuka na kusema kuna upotevu mkubwa wa fedha za serikali kutokana na msamaha wa kodi unaofanywa.
Taarifa zinasema kwamba Tanzania inapoteza Dola za Marekani 1.7 bilioni (Sh1.7 trilioni) kila mwaka kutokana na misamaha ya kodi, ukwepaji kodi na utoroshaji wa fedha na rasilimali nyingine nje ya nchi. Hakika mambo kama ni hivyo basi Watanzania tumekwisha! Kiwango cha fedha kinachotajwa kupotea, kingeweza kusaidia bajeti kuu ya serikali na kuondokana kabisa na taifa kuwa tegemezi kwa fedha za masharti wanazotoa wahisani.
Utafiti wa Kamati ya Viongozi wa Dini ya Masuala ya Uchumi na Haki za Binadamu (ISCJIC), umebainisha baadhi ya mambo yanayochangia upotevu huo kuwa ni sera mbovu za serikali, uzembe katika kukusanya kodi na vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya watendaji serikalini.
Ni jambo la kusikitisha na naomba wabunge chini ya Spika Anne Makinda walione hili wakati huu wa kujadili bajeti ya serikali ya mwaka 2012/ 13 inashangaza wananchi tunapoambiwa (na viongozi wanajua) kwamba baadhi ya kampuni, zikiwamo za madini zinazofanya kazi hapa nchini hazitozwi kodi kulingana na uzalishaji, jambo linalofanya zaidi ya nusu ya kodi wanazolipa kuwa ni zile zinazotokana na mishahara ya wafanyakazi wao.
Nizungumze na wabunge kwa kuwaambia kuwa kilio hiki cha upotevu wa fedha kwa njia hii siyo jambo jipya na linaweza lisiwe la kushangaza masikioni mwenu na hata Watanzania wengine kwa kuwa limekuwa likilalamikiwa mara kwa mara na watu wa kada mbalimbali.
Kinachoshangaza ni kuona Bunge ambalo ndilo linapaswa kuisimamia serikali limekaa kimya bila kutatua tatizo hili linaloangamiza taifa. Ukimya wa chombo hicho cha kutunga sheria katika eneo hilo nyeti uko wazi licha ya serikali kupoteza fedha nyingi ambazo zingesaidia kusukuma mbele maendeleo na kupunguza umaskini kwa wananchi.
Niseme wazi kuwa hatua ya kwanza ambayo wabunge wanapaswa kuchukua ni kuhakikisha mapato ya serikali yanaongezeka kwa kuisimamia serikaki ifanye vyema katika eneo hilo. Nakumbuka katika Bunge la Bajeti la mwaka 2011/12, Kambi ya Upinzani Bungeni ilipiga kelele sana kuhusu jambo hili wanalolilalamikia viongozi wa dini lakini hatujaona lolote lililofanyika, badala yake kilio hicho kimeendelea kusikika tena mwaka huu.
Tayari wiki iliyopita, Waziri Kivuli wa Fedha kutoka Kambi ya Upinzani, Zitto Kabwe alitaja vipaumbele katika bajeti yake mbadala, likiwamo suala la kupunguza upotevu wa fedha katika misamaha ya kodi kutoka asilimia tatu hadi asilimia moja.
Zitto alisema misamaha ya kodi inayotolewa kwa sasa ni mikubwa, sawa na misaada yote kutoka nchi wahisani ambayo ni Shilingi trilioni 1.03, kiwango ambacho kinawiana na utafiti wa viongozi wa dini. Ukweli kama ni huo ni kwamba tusipotoa misamaha hatutahitaji misaada kutoka nje.
Binafsi sioni sababu ya serikali kuendelea kuyafumbia macho maoni haya ya viongozi wa dini na kambi ya upinzani, hasa katika suala hili ambalo naamini ni muhimu kwa ustawi wa jamii yetu. Kinachotakiwa ni kuwepo kwa mipango mizuri ya kukusanya kodi, kupanua wigo, kudhibiti kampuni zinazokwepa kodi na kupunguza kwa kiwango kikubwa misamaha ya kodi kama si kuifuta kabisa ikiwezekana.
Litakuwa ni jambo la kushangaza kama serikali yetu itaendelea kuikumbatia misamaha hiyo kama ambavyo imekuwa ikifanya siku zote hasa baada ya kuwepo kwa taarifa za kuaminika kuwa wengi wanaonufaika na misamaha hiyo ni baadhi ya watendaji wachache ndani ya serikali wanaotumia madaraka yao vibaya kwani inadaiwa wanaipigania misahama hiyo ya kodi kwa makampuni hasa ya kigeni kwa sababu za ugonjwa mbaya wa rushwa.
Lakini siyo baadhi ya wabunge tu walioona kuwa katika eneo hilo kuna tatizo kwani hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh katika ripoti yake aliyoitoa alisema eneo hilo la misamaha ya kodi linapaswa kutazamwa ili kuepuka kuwa na makusanyo pungufu ya kodi ambazo husaidia sana uendeshaji wa nchi.
Niungane na Ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali na wadau wote wanaopigania suala hili, kuishauri serikali yetu kutazama njia nyingine ya kuvutia wawekezaji badala ya hii ya misamaha mikubwa ya kodi ambayo inawaumiza wananchi.
Maofisa wanaofanya vitendo hivyo, hasa kama wanakula rushwa, wajione kuwa ni wasaliti wa nchi hii na wajirekebishe.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
    Story na Shigongo

No comments:

Post a Comment

SHARE

TOA MAONI YAKO KUHUSU POST HII

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...