Thursday, April 11, 2013

LADY JAY DEE ANA KILA KITU!

MNYONGE mnyongeni lakini haki yake mpeni! Shikamoo Lady Jaydee. Salamu hii ni ishara ya kuunga mkono mafanikio ambayo ameyapata mwanamuziki huyu mkongwe wa Bongo Fleva, Judith Wambura Mbibo a.k.a Lady Jaydee, Jide, Komando na sasa anajiita Anaconda huku akilitupilia mbali lile la Binti Machozi akiseme; ‘I’m no longer Binti Machozi’.

Judith Wambura Mbibo a.k.a Lady Jaydee.

Achilia mbali hoja na mabishano ya juzikati kwenye mitandao ya kijamii kati yake na wanamuziki wengine wa muziki huo, zote ni changamoto za kimaisha. Haziepukiki. Siku zote mti wenye matunda ndiyo unaopigwa mawe.

ALIKOTOKEA Jide alianza kuimba kwenye Kwaya ya Kanisa la Kisabato, Magomeni, jijini Dar. Alipoingia kwenye Bongo Fleva alianzia kwa kurap kabla ya kufanya usaili wa utangazaji kwenye Kituo cha Redio cha Clouds FM ambapo alitusua vyema na kuanza kutangaza. Hapo ndipo Watanzania wengi walipoanza kumsikia.

...Gari kwa ajili ya bendi yake ya Machozi.

Kuelekea kuongeza ufundi na kulisaka soko la muziki, Jide alibadilika na kuanza kuimba RnB na ulipomkolea, aliamua kuachana na utangazaji na kujikita kwenye muziki peke yake. Muziki ulikua, akafanikiwa kutoa albamu kadhaa kabla ya kufikia hatua ya kumiliki bendi yake ya Machozi ambayo ilimuweka kwenye nafasi nzuri ya kutambulika ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Heshima ikaongezeka na sasa ana kila kitu. Kazi na dawa, safari nzuri ya maisha ya muziki isiyokuwa na skendo ilimpa heshima zaidi baada kufunga ndoa na mtangazaji maarufu Bongo, Gardner Gabriel Fikirini Habash ‘Kapteiiini’. Ndoa yao iliyodumu kwa takriban miaka nane sasa, pia ni chachu na fundisho kwa baadhi ya mastaa wanaochipukia kujifunza heshima ya ndoa.

... Nyumba anayoishi.

Bidii ya kujitanua kibiashara ndiyo ilisababisha mwaka 2010 afikie makubaliano na Kampuni ya Mohamed Enterprises kuzalisha maji yenye nembo ya jina lake ingawa biashara hiyo haikudumu kwa muda mrefu. Hakukata tamaa, cheche zake kwenye ujasiriamali zilizaa matunda kwenye mgahawa wake wa Nyumbani Lounge uliopo Ada Estate, Kinondoni, jijini Dar ambao unamuingizia mkwanja hadi sasa. Heshima kwake ilizidi kuongezeka, taratibu alifanikiwa kujijenga katika maisha yake binafsi kama ujenzi wa nyumba yake ya kifahari iliyopo Kimara, Dar. Mali kama magari ya kutembelea, magari ya kazi zake za muziki havimpigi chenga. Katika kuonesha muziki na ujasiriamali kwake vimevuka mipaka, ilifika wakati walishauriana na mumewe aachane na kazi ya utangazaji kwa muda ili aweze kusimamia miradi yao ambayo ilihitaji kutanuka zaidi jambo ambalo limefanikiwa.

...Akiwa kwenye gari lake aina ya Nissan Murano.

Safari ya kujitanua kibiashara haikuishia hapo, aliona kuna sababu ya kuanzisha kipindi chake cha runinga ambacho kina maudhui ya maisha yake halisi. Kinaitwa Diary ya Lady Jaydee kinachorushwa na runinga ya EATV. Kupitia hapo ameweza kupata faida mbili kwa wakati mmoja. Watu wengi wanazidi kumfuatilia (umaarufu unaongezeka), wakati huohuo anaingiza fedha kwa kukirusha kipindi hicho kinachodhaminiwa na kampuni kubwa ya simu za mikononi. Wasanii wanaochipukia kama akina Recho wa THT na wengine wengi wanapoona mafanikio kama haya, inawapa moyo wa kukaza msuli ili baadaye na wao waje kurithi nyayo za Jide. ‘Shikamoo’ nyingine inakuja kufuatia taarifa za chinichini kwamba mwanamuziki huyo anayetamba kwa sasa na wimbo wa Joto Hasira aliomshirikisha legend Profesa Jay, yuko mbioni kuanzisha kituo chake cha redio. Kama hivyo ndivyo, Lady Jaydee atakuwa ni mwanamuziki wa kwanza wa Bongo ambaye amethubutu kufanya makubwa ambayo kwa wasanii wengi itabaki kuwa ni ndoto kufikia.

...Ndani ya mgahawa wake wa Nyumbani Lounge.

ALBAMU ZAKE Hadi sasa, Jide anajivunia kuwa msanii aliyeweza kutengeneza albamu tano ambazo zina ujazo mkubwa wa ujumbe kwa jamii kama ile ya Machozi (2000), Binti (2003), Moto (2005), Shukrani (2007) na Ya Tano aliyoitoa mwaka jana.

KUHUSU TUZO Jide anajivunia kushinda Tuzo za Tanzania, Kilimanjaro Music (2004) kupitia kipengele cha Albamu Bora ya R&B (Binti), mwaka 2006 kupitia Tuzo za Pearl of Africa Music alizoshinda kama Mwanamuziki Bora wa Kike kutoka Tanzania. Kama hiyo haitoshi, mwaka 2007, Jide alishinda Wimbo Bora wa kushirikiana (Hawajui) kupitia Tanzania Music Awards alioshirikiana na MwanaFA.

...Akiwa na baadhi ya tuzo zake.

Mwaka 2008, kupitia Tanzania Music Awards, Lady Jaydee alishinda Tuzo ya Mwanamuziki Bora wa Kike pamoja na za Pearl of Africa Music katika kipengele hichohicho, Kisima Music Awards (Wimbo Bora wa Mwaka) uitwao Anita alioshirikiana na Matonya. Mwaka 2009, alishinda Tuzo za Tanzania Music (Wimbo Bora wa Mwaka), Anita kisha 2010 Tanzania Music Awards (Mwanamuziki Bora wa Kike), mwaka 2011 Mwanamuziki Bora wa Kike na Wimbo Bora wa Afrika (Nitafanya, aliomshirikisha Kidum kutoka Kenya na mwaka jana (Mwanamuziki Bora wa Kike).

No comments:

Post a Comment

SHARE

TOA MAONI YAKO KUHUSU POST HII

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...