Monday, April 22, 2013

AJALI LA ROLI,LATINGA MPAKA CHUMBANI LAUA WATATU.

LORI aina ya Scania limeingia chumbani katika nyumba moja kijijini Ilonga, wilayani Mbarali Mkoa wa Mbeya na kuua watu watatu wa familia moja waliokuwa ndani. Tukio hilo lilitokea Jumatatu iliyopita saa tatu na robo usiku ambapo Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, Barakael Masaki amethibitisha na kuwataja marehemu kuwa ni Asia Yahya (52), wanafunzi wa Shule ya Msingi Ilonga, Abubakari Yahaya (8) na Fatuma Yahaya (6). Kamanda Masaki ameongeza kuwa ajali hiyo ilihusisha malori mawili yaliyogongana kisha moja kugonga nyumba na kusababisha vifo vya watu hao na majeruhi ambao ni Abuu Fadhil (22) na Steven Chiwa (26) ambao wamelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Chimala. Alisema chanzo cha ajali ni gari lenye namba za usajili T578 ALS likiwa na tela lenye namba za usajili T125 AGM aina ya Scania kuligonga kwa nyuma gari lenye namba T959 ASC ambalo pia ni aina ya Scania. Alisema gari namba T959 ASC lilikuwa likiendeshwa na Juhudi Saimon (34), mkazi wa Dar es Salaam na ndilo lililogonga nyumba, mali ya Matia Mwagala mkazi wa Kijiji cha Ilongo ambayo marehemu walikuwa ndani. Hata hivyo, dereva wa gari lililosababisha ajali alikimbia na gari mara baada ya tukio ambapo Kaimu Kamanda anatoa rai kwa yeyote mwenye taarifa juu ya mahali alipo dereva wa gari lililosababisha ajali hiyo atoe taarifa kwani anatafutwa na polisi.

No comments:

Post a Comment

SHARE

TOA MAONI YAKO KUHUSU POST HII

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...