Tuesday, February 5, 2013

MFANYA BIASHARA AMPIGA MTU RISASI

MFANYABIASHARA wa mbao jijini Dar Salaam, Chacha Karongwe ‘Amang’ana’, wiki iliyopita alimpiga risasi kijana mmoja aliyetambulika kwa jina la Frank Filus, mkazi wa Tandika Mtaa wa Nasi B, kisa  kikitajwa ni  shilingi 100 inayodaiwa haikulipwa kwa ajili ya maji.
Frank Filus aliyepigwa risasi na mfanyabiashara wa mbao, Chacha Karongwe.
Majeruhi huyo aliyelazwa katika Hospitali ya Temeke, wodi na 7 alipohojiwa na gazeti hili alisema chanzo cha hayo yote ni shilingi 100 ambayo mama yake aliambiwa hajailipa kwa mke wa mtu aliyempiga risasi kutokana na maji aliyochota kwake.
“Mama yangu anayeitwa Sara Mwakatale alikwenda kuchota maji saa 12 jioni na hapakuwa na mtu wa kupokea fedha na kaacha  shilingi mia moja pale bombani, mara nyingi ndivyo tunavyofanya.
“Baadaye mama mwenye maji alimtolea maneno mabaya mama na akamuita mumewe ambaye naye alifanya kama mkewe, hali iliyomshangaza mama ambaye alimuuliza kwa nini anaingilia mambo ya wanawake.
“Mama alinipigia simu akanieleza mkasa nikarudi nyumbani, maelezo yake yalinifanya nimfuate Chacha  ambaye aliniambia kuwa alikuwa ananitafuta siku nyingi ndipo aliingia ndani na kutoka na bastola.
“Alipiga risasi moja ikanikosa shingoni, ya pili ikapita hewani lakini ya tatu ikanipiga pajani na kunivunja na hadi hivi sasa risasi hiyo haijatolewa,” alidai Frank.
Gazeti hili lilikwenda eneo la tukio na kukutana na Mjumbe wa Shina namba 45, Tandika Kilimahewa,  Rajabu Zuberi ambaye alisema kuwa wakazi wa eneo hilo wamesikitishwa  na tukio hilo kwa sababu haijawahi tokea mtaani kwao, kwanza  ni tukio la aibu mtu kupigwa risasi kwa sababu ya shilingi 100.
Kwa upande wa mke wa anayedaiwa kupiga risasi, Felistiana Chacha alisema kuwa mama Frank alichota maji bila kulipia shilingi 100 na alipomtuma mtoto kudai mama huyo alirudi na kumtukana hivyo akaenda Kituo cha Polisi Tandika Kilimahewa alikofungua kesi yenye jalada namba CHA/RB/792/2013 Lugha ya matusi na mtuhumiwa akakamatwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englebert Kiondo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema upelelezi unaendelea.

No comments:

Post a Comment

SHARE

TOA MAONI YAKO KUHUSU POST HII

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...