Wednesday, September 26, 2012

RICH KUOZEA JELA


Single Mtambalike ‘Rich'.

TUHUMA zinaonesha kwamba muigizaji Single Mtambalike ‘Rich’  amezoea kupiga wenzake na kuwajeruhi lakini tukio la sasa linaweza kumfanya aozee jela.
Kwa sasa, Rich anatuhumiwa kumpiga na kumjeruhi, mpigapicha za video wa Televisheni ya Taifa, TBC1, Moses Friday.
Kwa mujibu wa Friday, Rich amemkongoa meno saba na kumvunja taya, hivyo kumsababishia maumivu makali ya kinywa.
Habari zinasema kuwa Rich alichukizwa na kitendo cha Friday kumpiga picha, hivyo akaamua kumvaa, akampiga ngwala kabla ya kumshushia ngumi mfululizo zilizomsababishia akongoke meno na kuvunjika taya.
Awali, chanzo chetu kilisema kuwa Friday na Rich walikutana Sinza, Mapambano, Dar es Salaam, nyumbani kwa muigizaji, Gladys Chiduo ‘Zipompa’.
“Zipompa alikuwa anamtoa mwari ambaye ni mtoto wa ndugu yake. Akawaalika watu mbalimbali. Vilevile kulikuwa na muziki. Rich alifika akiwa na muigizaji mwenzake, Mayasa Mrisho ‘Maya’, wakati wa muziki wakawa wanacheza pamoja.
“Watu wakashangilia, wakamwambia Friday apige picha kwa sababu alifika kwenye shughuli hiyo kwa ajili ya kurekodi mkanda wa video ambao utatumika kwenye vipindi vya burudani TBC1.
“Kwa kawaida, Friday ndiyo mtayarishaji na muongozaji wa Kipindi cha Ben & Mai Live kinachorushwa moja kwa moja kila Jumamosi TBC1,” kilisema chanzo chetu.
Waandishi wetu walikutana na Friday, Jumamosi iliyopita alasiri, akiwa Hospitali ya Aga Khan ambapo alisema: “Nina maumivu makali, hapa nilipo nimeshazunguka hospitali tatu, nakosa ‘pleti’ kwa sababu taya limevunjika.
“Hapa pia hakuna pleti, kwa hiyo natakiwa kurudi Muhimbili. Ameniumiza sana, nitahakikisha sheria inachukua mkondo wake. Tayari nimesharipoti polisi, jalada lipo kwa namba KJN/RB/7732/2012.”
Jumapili iliyopita, waandishi wetu walimfuatilia na kubaini kwamba Friday alilazwa Muhimbili, akiendelea kupatiwa matibabu, wakati Rich alikuwa hajakamatwa.
Waandishi wetu walimtafuta Rich bila mafanikio, huku ikidaiwa kwamba alikuwa amejificha kukwepa mkono wa Jeshi la Polisi.
Mwaka jana, Rich aliwahi kumpiga muigizaji mwenzake wa kike, Colletha Raymond na kumjeruhi vibaya.
Colletha, alimripoti Rich Kituo cha Polisi Pangani Ilala, Dar es Salaam lakini kabla ya kufika mbali waliamua kusuluhisha nje ya mahakama.

No comments:

Post a Comment

SHARE

TOA MAONI YAKO KUHUSU POST HII

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...