Tuesday, September 4, 2012

MBONGO AZUA KASHESHE MAREKANI

Mwandishi Wetu
MTANZANIA aliyejulikana kwa jina moja la Patricia, mkazi wa jijini Dar es Salaam ambaye kwa sasa anaishi Texas, Marekani hivi karibuni alijikuta akizua kasheshe nzito kufuatia kuanguka chini na kurusharusha miguu kwa kile kilichodaiwa ni mapepo, Uwazi limepekenyua.
Katika DVD ya mahubiri ya mkutano mkubwa wa Kanisa la Synagogue Christian Of All Nations ‘SCOAN’ la Nabii T. B. Joshua wa Nigeria ambaye alizuru nchini Marekani hivi karibuni, Patricia alifika kuombewa kama waumini wengine lakini cha ajabu mapepo yakampiga mwereka.
Katika DVD hiyo, Patricia ambaye maandishi madogo chini ya DVD hiyo yalithibitisha yeye ni Mtanzania aishiye Marekani, alianza kwa kumjia juu Mtumishi wa Mungu, Wise Man Harry akitaka kupambana naye.
Hata hivyo, mtumishi huyo akilitumia jina la Yesu Kristo, alimmudu Patricia kiasi cha kumfanya aanguke chini kwa mwereka mzito kama mzigo huku kaumu ikimwangalia.
Kabla ya mwereka huo, Patricia kupitia mapepo ‘yake’ alisema alimuua baba yake mzazi na kwa wakati huo alikuwa akitaka kumuua mama yake mzazi ambaye alikuwa kitandani akiugulia tatizo la ini.
Akasema tatizo hilo yeye ‘pepo’ ndiye aliyeliingiza kwa mama wa Patricia kwa kuwa mwanamke huyo alikuwa akijifanya anaweza kusali kwa Mungu wake.
Hata hivyo, baada ya kuangushwa na mapepo hayo kufuatia maombi ya Harry, Patricia alisimama na kukanusha yote aliyosema awali (kupitia mapepo).
Alisema anampenda sana mama yake mzazi, hawezi kumuua na pia baba yake alikuwa mwema sana hivyo asingeweza kumuua kwa sababu yeye hana uwezo huo.
Mtumishi Harry akamwambia roho chafu iliyokuwemo ndani mwake ndiyo ilikuwa ikisema hayo, imeshaondoka na hata mama yake yuko sawa maneno ambayo yalimfanya mrembo huyo kufurahi.
Katika mahubiri hayo, Wamarekani mbalimbali pia walipiga mwereka kwa mapepo ambapo baada ya kuombewa walirudia katika hali yao ya kawaida huku wakimshukuru sana Mungu.

No comments:

Post a Comment

SHARE

TOA MAONI YAKO KUHUSU POST HII

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...