Tuesday, September 18, 2012

MAMA AMFIKISHA MWANAYE POLISI, KISA MALI ZA URITHI


Bi. Basila Komu.
Nyumba ya urithi.
Stori: Haruni Sanchawa
MWANAMKE mmoja mkazi wa Mbezi Beach jijini Dar, Basila Komu hivi karibuni alimfikisha mwanaye wa kumzaa katika Kituo cha Polisi cha Kawe kufuatia mtoto huyo kung’ang’ania mali za urithi za baba yake kinyume na taratibu.
Akizungumza na Uwazi, mama huyo alidai kuwa mtoto wake huyo aliyemtaja kwa jina la Michael Komu amekuwa akimkosesha amani tangu mumewe afariki kwani kuna wakati alimfukuza kwenye nyumba yao akidai ni mali yake.
“Mimi ni mjane, hii nyumba ni mali ya marehemu mume wangu aliyefariki mwaka 2005 lakini nashangaa huyo mtoto anadai ni yake. Mbali na nyumba, kuna mali nyingi ambazo marehemu kaziacha ambazo mtoto huyu anadai anazimiliki yeye,” alidai mama huyo na kuongeza:
“Kwa kweli ananifanya niishi kwa hofu sana, anayofanya mtoto huyu ni ya kushangaza. Ameficha baadhi ya hati muhimu za mali kisha amehama na kwenda kuishi kwingine, kwa kweli naomba vyombo vya dola vinisaidie.”
Baada ya kuona mambo yanazidi kuwa mabaya, mama huyo aliamua kwenda kumripoti mwanaye huyo kwenye Kituo cha Polisi cha Kawe na kufungua kesi yenye jalada namba KW/RB/8863/2012.
Kwa upande wa Michael Komu ambaye kitaaluma ni mhandisi, alisema ni kweli Basila ni mama yake mzazi ila akadai yote yanayotokea ni kwa sababu mama huyo ana matatizo ya akili.
Akizungumzia sakata hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela alikiri tukio hilo kuripotiwa kwake na kwamba linafuatiliwa ili hatua zinazofaa ziweze kuchukuliwa.

No comments:

Post a Comment

SHARE

TOA MAONI YAKO KUHUSU POST HII

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...