Ureno imo katika robo fainali
Mabao mawili ya mshambulizi Cristiano Ronaldo
yaliiwezesha Ureno kuingia robo fainali ya michuano ya Euro 2012, kwa
kuifunga Uholanzi, na pasipo shaka yoyote, kuwalazimisha kurudi
nyumbani.
Kwa Uholanzi kuwa na matumaini yoyote kuendelea
kusalia katika mashindano hayo, walilazimika kuifunga Ureno magoli 2-0,
na bao la kwanza la mkwaju wa kupinda kutoka kwa Rafael van der Vaart
liliwapa matumaini Uholanzi walipoweza kutangulia.
Lakini mchezo wa Uholanzi uliendelea kufifia, na Ronaldo alifanikiwa kusawazisha, alipopigiwa mpira na mwenzake Joao Pereira.
Nani alimsaidia Ronaldo kufunga kwa mara ya
pili, na Ureno ikavuka hatua ya makundi na kujiandikishia nafasi katika
robo fainali.
Ureno sasa itacheza na Jamhuri ya Czech, inayoongoza kundi A.
Kwa Uholanzi, timu hiyo imeonyesha mchezo duni
sana, kwa kushindwa katika mechi tatu za makundi, ilhali miaka miwili
iliyopita, wao walimaliza katika nafasi ya pili katika fainali ya Kombe
la Dunia nchini Afrika Kusini.
Itawachukua muda Uholanzi kumsahau Ronaldo,
mchezaji nyota wa Real Madrid ya Uhispania, ambaye aliifungia klabu hiyo
magoli 60 msimu uliopita, na katika mechi dhidi ya Jumapili alicheza
kwa kasi na kwa juhudi na kuwaacha Waholanzi wamezubaa.
No comments:
Post a Comment