Ahukumiwa jela maisha kwa kumuua Malkia
Mahakama ya kimataifa inayochunguza mauji ya kimbari
nchini Rwanda{ICTR} imemhukumu mwanajeshi wa zamani kifungo cha maisha
jela kwa kuhusika na mauaji hayo ya mwaka 1994.
Ildephonse Nizeyimana,alipatikana na hatia ya
kuamrisha mauaji ya aliyekuwa Malkia wa jamii ya Tutsi Rosalie Gicanda
pamoja na mauaji mengine.Nizeyimana alikamatwa nchini Uganda mwaka wa
2009.
Aliongoza kitengo cha ujasusi na operesheni za jeshi katika chuo cha mafunzo ya kijeshi cha ESO,wakati wa mauaji ya kimbari.
Mahakama hiyo iliyoko mjini Arusha, Tanzania
ilimpata na hatia mwanajeshi huyo wa zamani ambapo aliamrisha mauaji ya
raia kadhaa akiwemo malkia huyo wa Tutsi.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la kutetea haki
za binadamu Human Rights Watch mwaka wa 1999, wanajeshi wa Ki-Hutu
walimchukua Malkia huyo kutoka makaazi yake Kusini Mashariki katika mji
wa Butare na kisha kumpiga risasi nyuma ya jumba la makumbusho.
Pia waliwaua wanawake wakadhaa waliokuwa
wajakazi wa malkia huyo.Marehemu alikuwa mjane wa Mfalme Mutara III,
aliyefariki dunia mwaka wa 1959 kabla ya nchi hiyo kutangazwa jamuhuri.
Mahakama ya ICTR ilibuniwa kuwafungulia kesi
wafadhili na washiriki wa mauaji ya kimbari. Tayari imewahukumu watu 54
na kuwaachia huru wanane. Mahakama hiyo inafunga shughuli zake baadaye
mwaka huu.
No comments:
Post a Comment