Mchezaji wa Manchester United
Phil Jones atawekwa kando kwa muda wa wiki nane kufuatia kufanyiwa
upasuaji wa goti, kwa mujibu wa taaarifa zilizotolewa na klabu hiyo.
Jones,mwenye umri wa miaka 20, hakuweza kucheza
msimu huu baada ya kuumia mgongo wakati wa mechi za awali kabla ya msimu
na pia kuumia mguu uliopelekea upasuaji huo.
"Phil Jones amefanyiwa upasuaji wa mguu sehemu ya goti kufuatia kujeruhiwa wakati wa mazoezi," amesema msemaji wa United.
"Itachukua kati ya wiki sita hadi nane kuweza kupona."
Jones anasemekana kupata majeraha hayo mapema wiki hii wakati alipokuwa mazoezini.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa England alipelekwa
kufanyiwa uchunguzi wa sehemu ya goti la mguu wa kulia uliothibitisha
kuwa anahitaji mapumziko marefu kuweza kupona.
Jones alikuwa akitarajiwa kurejea ulingoni baada
ya mapumziko mengine ya kuuguza mgongo lakini matokeo yake ataendelea
na mapumziko zaidi.
Upasuaji huo huenda ukasababisha Jones kukosa
mashindano ya michezo ya makundi ya Champions League dhidi ya
Galatasaray yanayofanyika Septemba 19, na pia dhidi ya CFR Cluj-Napoca
tarehe 2 Oktoba na mechi ya tarehe 23 Oktoba na Braga.
Hali kadhalika atakosa mechi sita za Premier
League ikiwemo ile kati ya Manchester United na Liverpool Septemba 23 na
ya Chelsea tarehe 28 Oktoba.
Manager Sir Alex Ferguson anamatumaini kuwa
mchezaji huyo wa zamani wa Blackburn ataweza kushiriki mechi dhidi ya
Arsenal mnamo tarehe 3 Novemba.
No comments:
Post a Comment