TUKIO la kuuawa kikatili, Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, lina
mshindo mkubwa na hali halisi ilivyo ni wazi hatapona mtu kutoka kila
upande uliohusika.
Habari zinasema kuwa namna tume iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya
Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, inavyotakiwa kufanya kazi, ni lazima
itaibuka na majibu yatakayowamaliza wahusika.
Risasi Jumamosi, limenasa taarifa kwamba kuna waandishi wa habari,
hususan wale waliokuwepo eneo la tukio siku Mwangosi anauawa, wamekuwa
wakipewa msukosuko ili kuwakata kilimilimi wasije wakanena mazito kwenye
tume.
Imebainishwa kuwa tayari baadhi ya waandishi wa habari waliokuwa
wanatafutwa mara kwa mara, wameshaondoka Iringa kupisha vuguvugu
linaloendelea kwa sasa mkoani humo.
Mwandishi mmoja (jina tunalo) aliliambia Risasi Jumamosi: “Iringa
hakukaliki. Kila mara tunapewa vitisho tujitokeze, sijui wanataka
kutufanya nini. Sisi tuko makini na kifo cha mwenzetu na tutakapoitwa
mbele ya tume, tutaeleza ukweli.”
Wakati tume hiyo ya Nchimbi inayoongozwa na Jaji Mstaafu, Stephen
Ihema ikianza kazi, inaelezwa kwamba itapitia sakata hilo kuanzia mwanzo
mpaka mwisho.
Mmoja wa wajumbe wa tume hiyo aliliambia gazeti hili kwa sharti la
kutotajwa jina: “Kuna mambo ya mwanzoni, wakati wa tukio na baada.
Maeneo hayo yote tutayaangalia kisha tutakabidhi ripoti ya tume yetu kwa
mheshimiwa waziri.
“Tume yetu inafanya kazi kwa mujibu wa sheria. Hata tulipoteuliwa,
hatujapewa muongozo wa kuficha baadhi ya mambo. Tunatakiwa kuchunguza
kiini na ukweli halisi. “Umakini wa tume yetu utajionesha baada ya
kukabidhi ripoti yetu.”
Alipoulizwa kuhusu kile walichokibaini katika hatua za awali,
alijibu: “Huo siyo utendaji mzuri. Sisi ni watu wenye maadili, siwezi
kusema tumeona nini hata kama yapo tuliyokwishayaona. Wewe fahamu tu
kwamba tupo kazini na majibu ya tume yataonekana kwenye ripoti ya
mheshimiwa waziri.”
Pamoja na ugumu wa kupata ‘a-b-c’ za awali ndani ya tume, imeelezwa
kwamba Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa na viongozi wa Chama cha
Demokrasia na Maendeo (Chadema), hususan Katibu Mkuu, Dk. Willibroad
Slaa, wana kazi ya kujieleza mbele ya tume hiyo.
Slaa, atajieleza pia mbele ya tume hiyo kwa sababu kabla ya siku ya
tukio, anadaiwa kupishana maneno na Jeshi la Polisi kuhusu amri ya
serikali iliyokataza mkusanyiko wa aina yoyote wa vyama vya siasa katika
kipindi cha sensa.
Habari zinasema pia kwamba viongozi wa Chadema Mkoa wa Iringa,
watahojiwa kwa sababu wao ni sehemu ya chanzo cha mkusanyiko
uliosababisha kifo cha Mwangosi wakati polisi walipokuwa wanawatawanya.
Inaelezwa kuwa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda
na askari wake, hasa wale waliotekeleza oparesheni ya kuwatawanya
Chadema, Kata ya Nyololo, Mufindi, watahojiwa na tume.
Sababu kuu ni kwamba, Mwangosi alifikwa na mauti akiwa katikati ya
polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na kumekuwa na tuhuma nyingi
zinazowahusisha polisi na kifo cha mwandishi huyo.
Mwangosi, aliuawa Septemba 2, 2012, Kijiji cha Nyololo, Mufindi
Iringa wakati wa vurugu za polisi dhidi ya wafuasi wa Chadema. Katika
tukio hilo, afande mmoja ambaye ni jirani na marehemu kwenye makazi
alijeruhiwa.
Imeelezwa kuwa, marehemu ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Klabu ya
Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, alilipukiwa na kile kinachodaiwa ni
bomu wakati akidhibitiwa na maafande wa Jeshi la Polisi.
Habari zinasema kwamba, Mwangosi aliingia kwenye zahama hiyo
alipokwenda kuwahoji polisi sababu ya kumkamata mwandishi wa Gazeti la
Nipashe, Godfrey Mushi.
No comments:
Post a Comment