Idadi kubwa ya watu wameripotiwa
kufariki kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa siku nzima na kusababisha
mafuriko katika mji mkuu wa Ufilipino, Manila.
Mafuriko hayo ambayo yamesababisha athari kubwa
katika baadhi ya maeneo, yamewalazimisha maelfu ya watu kutoroka makwao
huku mashule, afisi za serikali na soko la hisa zikishindwa kuendelea na
shughuli za siku kutokana na maji yanayoaminiwa kufikia kiunoni.
Familia moja ya watu wanane waliangamia baada ya maporomoko ya ardhi kuangusha nyumba nyingi kwenye mitaa duni mjini Quezon.
Mvua zaidi inatabiriwa kunyesha katika siku mbili zijazo.
Mji wa Manilla na maeneo mengine kaskazini mwa
nchi hiyo zimekumbwa na hali mbaya ya anga tangu kutokea kimbunga cha
Saola yapata wiki moja iliyopita.
Kufikia sasa takriban watu hamsini wamethibitishwa kufariki kufuatia gharika iliyotokea wiki mbili zilizopita.
Mafuruko makubwa yanatabiriwa kutokea katika mji
mkuu na viunga vyake pamoja na mikoa mingine kulingana na taarifa ya
baraza la utabiri na udhibiti wa majanga nchini humo.
Kinachowatia wasiwasi watu wengi nchini humo ni
kuwa mvua imekuwa ikinyesha kwa masaa 24 na kwamba mvua kama hii ndiyo
iliyosababisha mafuriko baada ya kimbunga Ketsana mwaka 2009.
Wakati huu serikali inasema imejiandaa vyema
kukabiliana na hali hiyo na hadi sasa imeweza kuwahamisha maelfu ya watu
kutoka maeno yenye mafuriko.
Lakini watu wengi hawataki kabisa kuhama hasa
ikiwa hawawezi kuchukua mali zao,wengi wameonekana wakirejea kwenye maji
kwenda kwa nyumba kuweza kunusuru mali zao.
Rais Benigno Aquino tayari amekutana na maafisa
wa ulinzi kujadili mipango ya usalama na kwamba kila mtu ambaye ana
jukumu la ulinzi tayari wamejiandaa.
Maafisa wa serikali wamelazimika kutangazia watu
kuchukua hatua za dharura ili kujilinda kutokana na hatari zozote hasa
baada ya watu wanne kuripotiwa kufa maji katika mkoa mwingine ingawa
taarifa hizi bado hazijathibitishwa.
Wakuu wa utabiri wa hali ya hewa, wameonya kuwa
mafuriko huenda yakawa makubwa zaidi hasa baada ya bwawa kubwa la "La
Mesa" kufurika.
No comments:
Post a Comment