Zaidi ya watu mia moja
wamefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya lori la mafuta kuanguka
kusini mashariki mwa nigeria katika Jimbo la Delta.
Wakuu wa Serikali wanasema kuwa wenyeji wa eneo
hilo walikimbilia kuzoa mafuta yaliokuwa yakichuruzika toka lori hilo
lakini likalipuka na na kusababisha maafa hayo.
Mwandishi wa habari Emeka Idika ameiambia BBC
kuwa mazishi ya halaiki kwa watu waliofariki kutokana na moto na
wasioweza kutambulika yatafanywa katika Jimbo la Rivers wakati wengine
wapatao 35 wamelazwa katika hospitali.
Mwandishi huyo ameongezea kusema kuwa idadi ya
vifo huenda ikaongezeka kwa sababu kuna baadhi ya watu kutoka vijiji
vilivyo karibu na hapo Okogbe waliokua wamekumbwa na balaa la moto
mkubwa walikimbilia vichakani na miili yao bado haijaonekana.
Mwandishi mwingine , Oluchi Iwuoha Chimezie, ameiambia BBC kuwa alihesabu zaidi ya maiti 100.
Shirika la habari la Reauters limemnukuu msemaji
wa Polisi ya Jimbo la Rivers state, Ben Ugwuegbulam akisema kuwa
"mapema leo Lori lililobeba mafuta lilipinduka huko Okogbe na watu
kukimbia haraka kujizolea mafuta yaliyokuwa yakimiminika na ghafla bin
vuu moto ukalipuka na kusababisha madhara.
Taasisi inayosimamia usalama wa barabarani
imesema kuwa Lori hilo liligonga magari matatu. Matukio ya aina hiyo si
mageni nchini Nigeria.
Mamiya ya watu wamefariki katika kipindi cha
miaka kumi iliyopita wakijaribu kuchota mafuta kutoka mabomba yanayovuja
kwa sababu ya kuvunjwa makusudi au watu wanaojaribu kuiba mafuta.
Nigeria ni nchi inayozalisha na kuuza mafuta kwa kiwango kikubwa lakini mamilioni ya raia wake wanaishi maisha ya ufukara.
No comments:
Post a Comment