Mahakama nchini Namibia imetoa
uamuzi wake kuwa wanawake watatu wanaoishi na virusi vya HIV haki zao za
kibinadamu zilikiukwa walipofungiwa uzazi bila ridhaa yao.
Wanawake hao wanasema waliambiwa wafanyiwe
utaratibu huo kama walikuwa wanataka kujifungua kwa upasuaji kupunguza
uwezekano wa watoto wao kuambukizwa virusi vya HIV.
Mahakama hiyo iaangalia ni kwa namna
gani watapata fidia ya athari walioipata. Mwandishi wa BBC Kusini mwa
Afrika anasema uamuzi huo wa mahakama kuwapa haki wanawake hao unaweza
kuwa na athari chanya kwa nchini nyingine katika ukanda huo.
Kesi hiyo ilifunguliwa na wanawake wajawazito
watatu walioamua kujifungua kwa upasuaji ili kupunguza uwezekano wa
watoto wao kuambukizwa virusi vya HIV.
Maafisa wa afya wamekana kuwa wanawake hao walifungwa uzazi kwa nguvu bila ridhaa yao.
Mawakili wa wanawake hao wanasema kesi nyingine kama hizo zimeripotiwa katika nchi nyingine katika ukanda huo.
Awali mawakili wa wanawake hao walisema wateja
wao waliambiwa na madaktari nchini Namibia kuwa wangeweza tu kufanyiwa
upasuaji iwapo wangekubali kufungiwa uzazi kwa wati huo.
Mawakili hao wanasema kulazimishwa kukubaliana
ni tofauti na kupatiwa taarifa muhimu ili kukubalina na jambo hilo na
kwa hiyo mamlaka za Namibia zilikiuka haki za binadamu kwa wanawake hao.
Wizara ya afya inakanusha kuwa ilitoa maelekezo
kwa wanawake wanaoishi na virusi vya HIV wafungiwe uzazi na kuongeza
kuwa haikuwa inafahamu kuwa kuna mtu yeyote amefungiwa uzazi bila ridhaa
yao.
Nicole Fritz, kutoka kituo cha Sheria cha Kusini
mwa Afrika na hivyo kufungua kesi, ameiambia BBC kuwa wanawake hao
wamekuwa kwenye maumivu na hawajui nini kitatokea.
"Mmoja wa wanawake hao amekuwa kwenye uchungu
kwa siku nne, uchungu ambao hauelezeki. Wengine kati hao hawakujua hasa
kile walichokuwa wakikubaliana nacho. Walidhani ilikuwa ni sehemu ya
utaratibu wa kufanyiwa upasuaji,"Alisema
"Hivyo taarifa kuwa walikubaliana, hawakuelewa
kilichokuwa kinaendelea, hawakujua utaratibu ulivyokuwa na walikuwa
wanakubaliana na nini, hawakuwa na taarifa za kutosha kukubaliana. "
Mawakili wanasema wana ushahidi kuwa wanawake
wanalazimishwa kufungiwa uzazi nchini Swaziland na baadhi ya maeneo ya
Afrika Kusini, ambapo wanasema inawanyima wanawake hao haki zao za
kikatiba.
Kiasi cha 13% ya watu wazima nchino Nambia wanaishi na virusi vya HIV kwa mujibu wa UNAids.
No comments:
Post a Comment