Uwamuzi wa Mahakama kutomtia hatiani John Terry
kwa mashitaka ya kumtukana mlinzi wa QPR, Anton Ferdinand umepokewa kwa
hisia tofauti.
Mahakama
ya Westminster jijini London ilimkuta nahodha huyo wa Chelsea hana
hatia ya kumtukana Ferdinand kwa kutumia lugha ya kibaguzi timu zao
zilipokutana Loftus Road mwaka jana.
Terry mwenye umri wa miaka 31 alipoteza unahodha
wa timu ya taifa ya England kwa sababu ya kisa hicho kilichokuwa bado
kinachunguzwa na Polisi.
Wakati wote, kabla na katika kesi, Terry amekuwa akikanusha madai hayo, ambapo kuachiwa kwake kumepokewa kwa furaha kubwa na wana Chelsea.
Pamoja na kuachiwa kwa Terry, bado sakata zima
halijaisha, kwani tayari Chama cha Soka cha England kimeanza uchunguzi
wake juu ya tukio zima. Kilisitisha hatua zake ili kupisha hatua za
kipolisi na mahakama zilizohitimishwa Ijumaa.
Kama ilivyo katika soka, mechi huwa na nusu
mbili zinazoifanya kuwa na jumla ya dakika 90, sakata la Terry
linachukuliwa limefika dakika 45 za kwanza.
Taarifa ya FA ilitolewa mara baada ya Terry kutotiwa hatiani. Suala hilo katika ujumla wake limeitia aibu kandanda.
Afisa Mtendaji wa Chama cha Wacheza Soka wa
Kulipwa (PFA), Gordon Taylor amenukuliwa akisema sura ya mchezo huo
imeathiriwa vibaya na sakata hilo na kutaka kampeni ya 'Respect' ienziwe
vyema.
Baada ya mahakama kuacha wazi milango kwa FA, kuna uwezekano wa kutoa tamko zito na kuchukua hatua.
Hii ni kwa sababu FA haibanwi kisheria kuwa na
ushahidi wa kutosheleza pasipo shaka, bali ni kwa kuangalia tu mantiki
na urari wa uwezekano wa jambo hilo kuwa limetokea.
Hii ni tofauti kabisa na kwenye kesi ya jinai,
ambapo lazima ushahidi upembuliwe, uchujwe na kupimwa ili mahakama iweze
kujiridhisha pasipo chembe ya shaka kwamba mhusika alitenda kosa.
Kisheria, katika jinai inashauriwa (na ni rahisi zaidi) mkosaji
kuachiliwa huru pale panapotokea utata wa iwapo alitenda kosa au la
kuliko kumtia hatiani katika mazingira hayo.
Mdhamini wa wakfu wa 'Kick It Out' unaopambana
na ubaguzi wa rangi michezoni, Garth Crooks anasema sakata la Terry bado
ni bichi kabisa.
Crooks aliyepata kuwa mwenyekiti wa PFA, anasema
kwamba Terry bado yupo chini ya uchunguzi wa chama cha soka, kwa
kuzingatia kile alichokiri - kusema maneno fulani. Nadhani kwa Terry
haya ni mapumziko ya muda tu, mambo hayajaisha…kitu kinachokuwa kigumu
kueleweka katika soka ni kwamba kuna kizazi kizima cha wachezaji weusi
wanaojihisi kwamba mchezo huu umewakwaza.
"Hawatakubali kutukanwa kibaguzi tena, iwe na
wachezaji au washabiki. Ikiwa Chama cha Soka hakifanyi kitu licha ya
kuwa na ushahidi tayari, basi mwangwi wake kwenye mchezo huu utakuwa na
athari kubwa kwa miaka mingi ijayo," anasema Crooks.
Terry anaonekana kama mtu asiyetishika wala
kuguswa, kwa sababu amefanikiwa kutoka mweupe kwenye kashfa kadhaa
kubwa, akichanja mbuga katika soka yake bila wasiwasi.
Pengine kadiri mambo mengi yanavyozidi kumwandama atakuwa amepata funzo hata kama si kuadhibiwa moja kwa moja.
Ukimwacha Terry, soka kwa ujumla inaanza kuonekana kana kwamba ni kitu kilichojitenga na jamii, kwa jinsi watu wanaoonekana wazi kufanya makosa wanavyoachiwa.
Ukimwacha Terry, soka kwa ujumla inaanza kuonekana kana kwamba ni kitu kilichojitenga na jamii, kwa jinsi watu wanaoonekana wazi kufanya makosa wanavyoachiwa.
Wapo wanaofikiria kwamba ingekuwa ni mtu fulani
ofisini amemtukana mwenzake kwa kutumia lugha ya kibaguzi, angefukuzwa
moja kwa moja au kupigwa marufuku utumishi kwenye nafasi kama aliyokuwa
nayo.
Chelsea nayo wakati wote imeelekea ama kumbeba
Terry au yeye kuiganda klabu akiwa na bendera inayomwonesha kuwa ndiye
nahodha, kiongozi na mkongwe wa Stamford Bridge.
Haikupata kutokea, isipokuwa katika kesi hii ya
Terry, mahakama kujiingiza kwa undani kuchunguza nini huwa kinatokea
kwenye mechi za hadhi ya juu, ikaanikwa wazi jinsi inavyoharibu, kutia
aibu, kukasirisha na mara nyingi zaidi kuumiza.
Terry anaweza kuchukulia kwamba huu ni ushindi
wa aina fulani, lakini mchezo kwa ujumla wake umeathiriwa kwa kiasi
kikubwa. Kwa hakika hii ni sumu mchezoni, ambayo inaweza kusemwa kwamba
imezama hadi kwenye mizizi yake. Inahitajika kazi kubwa sana kumaliza
ubaguzi mpirani, na daima mdudu huyu ataendelea kuwaweka hadharani
walengwa wake wakubwa hadi watakapotia adabu.
Ni bahati mbaya kwamba sasa inaelekea
hatuzungumziii wala hatujajikita tu kwenye matumizi ya lugha mbaya, bali
kujiimarisha katika kujenga uadui wenye misingi yake katika mifupa,
sijui kwa faida ya nani.
Ni muhimu kutambua kwamba katika hili hapawezi
kuwapo washindi na washindwa, kwani soka ndiyo inatakiwa kuendelezwa,
haya mengine yote yanaizorotesha na kuichafua hadhi yake.
Ukiachilia mbali uwamuzi wa hakimu yule, kilicho
dhahiri ni kwamba soka ya England imejikuta katika ulege lege wa aina
yake, kila mmoja akipoteza badala ya kupata.
No comments:
Post a Comment