Hakika kila chenye mwanzo hakikosi mwisho, na kila mwisho wa jambo moja
huwa mwanzo wa jingine. Ingawa huenda ni mapema sana kwangu kutoa
tafakuri kamili ya muhula wangu katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa, hapana shaka kabisa kuwa nafasi hiyo imenipa uzoefu
maridhawa. Namshukuru Katibu Mkuu BAN Ki-moon kwa kunipa fursa hii,
kuniamini na kwa ushirikiano mkubwa wakati wote wa utumishi wangu.
Kukitumikia chombo hiki cha kimataifa kwa muda wa miaka mitano na
nusu mfululizo ni heshima ya pekee ambayo daima nitaienzi kama kilele
kimojawapo cha maisha yangu ya utumishi wa umma. Kila siku niliyoitumia
katika Umoja huo ilikuwa ni darasa la kusukuma mbele mipaka ya ujuzi na
elimu. Nimepata kufahamu mengi zaidi kuhusu Shirika lenyewe; kuhusu
dunia na watu wake, lakini pia kufahamu ukomo wa uwezo wa Umoja wa
Mataifa katika kushughulikia changamoto mbali mbali zinazoikabili dunia
yetu.
Utumishi wangu katika Umoja wa mataifa ulikuwa fursa adhimu iliyonipa
uzoefu wa pekee. Kazi hii imeujaza moyo wangu na unyenyekevu wa dhati
kwani niliingia Umoja wa Mataifa wakati ambapo dunia inachagizwa na
madhila makubwa makubwa yakiwemo maradhi, umaskini wa kupindukia,
kutokuwapo kwa usawa wa kijinsia, kuongezeka kwa vitendo vya ukatili na
udhalilishaji kwa wanawake na watoto; na changamoto nyingine nyingi. Kwa
muktadha huu ilikuwa fursa ya pekee kuchangia juhudi za pamoja za
kuimarisha Umoja wa Mataifa katika kutekeleza majukumu yake katika
kipindi cha mazingira magumu ya kimataifa yaliyojaa changamoto za
kipekee kabisa.
Daima nitaendelea kushukuru na kuthamini kwa dhati jinsi Mhe. Rais
Jakaya Mrisho Kikwete, Serikali na Watanzania wenzangu walivyonitia moyo
na kunienzi katika kipindi chote nilichokuwa Umoja wa Mataifa. Familia
yangu, ndugu na marafiki walikuwa karibu nami kwa dua na kunitia nguvu
wakati wote wa utumishi wangu. Nawashukuru sana.
Hapana shaka kazi yangu katika Umoja wa Mataifa imeniwezesha
kufahamiana kwa karibu na viongozi wengi wa kimataifa na pia watu mbali
mbali waliopata mafanikio makubwa duniani. Nimeweza kufahamu kwa undani
thamani ya michango yao katika kujenga amani na ustawi wa dunia.
Zaidi ya yote, sitasahau hisia nilizopata kila nilipokutana na watu
wanyonge waliokuwa wanahitaji msaada wa Umoja wa Mataifa. Nitakumbuka
daima tabasamu ya mwanamke mmoja niliyekutana naye katika moja ya ziara
zangu barani Afrika nilipotembelea zahanati mojawapo kati ya kadhaa
zinazofadhiliwa na Umoja wa Mataifa. Mama huyo mwenye watoto sita,
alikuwa amekikumbatia kitoto chake kimoja kilichokuwa nyonde nyonde;
lakini alikuwa na tabasamu iliyojaa faraja na matumaini kwa kuwa alikuwa
amefanikiwa kupata bure dawa za kunusuru maisha ya mwanawe.
Maendeleo
Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliasisiwa na
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1997 kwa madhumuni ya kuongeza
ufanisi wa utendaji wa Sekretariati na kuimarisha uongozi wa Umoja
Mataifa katika medani za uchumi na maendeleo ya jamii. Majukumu ya
Naibu Katibu Mkuu yaliongezeka kadri Shirika lilivyokuwa linapanua
shughuli zake. Hatimaye Naibu Katibu Mkuu akakabidhiwa jukumu la
kuoanisha na kuratibu idara zote zilizo chini ya mwavuli wa Umoja wa
Mataifa. Jukumu hili lilikuwa na manufaa makubwa, hususan tulipoingia
katika utekelezaji wa dhana ya “Huduma ya Pamoja ” (Delivering as One –
DaO) ili kuleta ufanisi zaidi katika kazi zetu hususan za maendeleo.
Kwa bahati nzuri, ninamaliza kipindi changu kukiwa na maendeleo
mazuri yanayotokana na jitihada za kimataifa za kupambana na umaskini.
Takwimu za kuaminika za hivi karibuni zinatuambia kuwa juhudi zetu za
kupunguza idadi ya watu maskini duniani kufikia angalau nusu ya viwango
vya sasa zimeanza kuzaa matunda. Taarifa hii ni ya kutia moyo licha ya
ukweli kwamba dunia inapitia dhahama kubwa ya kiuchumi kuliko wakati
mwingine wowote katika miaka ya hivi karibuni. Pamoja na majukumu
mengine,nguvu zetu tulizielekeza zaidi kwenye kufanikisha malengo ya
maendeleo ya milenia na malengo mengine ya maendeleo yaliyokubaliwa
kimataifa. Nilihamasika sana na dhamira waliyoionesha wadau na washirika
wetu wa maendeleo: serikali, mashirika ya kiraia na mashirika ya
biashara. Kwani wote kwa pamoja waliyatumia malengo hayo kama kilingo
cha msingi katika kutokomeza umaskini.
Katika kufanikisha utekelezaji madhubuti wa malengo ya maendeleo ya
milenia nilipewa jukumu la kukamilisha ahadi ya Katibu Mkuu aliyoitoa
kwa nchi wanachama ya kuunda Mfumo Kamilifu wa Utekelezaji wa Malengo ya
Maendeleo ya Milenia (MDGs Integrated Implementation Framework ).
Ninaona fahari kwamba naondoka Umoja wa Mataifa mfumo huu ukiwa
umekamilika ambapo Katibu Mkuu aliuzindua mwezi Juni mwaka huu. Kwa mara
ya kwanza mfumo huu umeweka utaratibu ambao utauwezesha Umoja wa
Mataifa na wadau wote kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa ahadi za
kisera na kifedha. Hapana shaka utaratibu huu utaongeza uwajibikaji wa
wadau na upimaji sahihi wa hatua za maendeleo.
Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) Barani Afrika
Kwa mwelekeo huo huo, Katibu Mkuu alizindua Jopo la Viongozi la
Kuhimiza Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia Barani Afrika
(MDG Africa Steering Group) mwezi September 2007. Kikundi hiki
kinajumuisha taasisi zote kuu duniani zilizo mstari wa mbele katika
kuchochea kasi ya maendeleo ya Afrika. Nilipata bahati ya kukiongoza
kikosi-kazi (MDG Africa Working Group) kilichokuwa mhimili wa Jopo hilo
la viongozi. Baada ya miaka mitano ya majadiliano ya kina, Jopo hilo
likiongozwa na Katibu Mkuu limetoa mapendekezo kamambe ya utekelezaji.
Endapo mapendekezo haya yatazingatiwa basi yatakuwa nyenzo muhimu ya
kuweka sera na mikakati madhubuti itakayosaidia maendeleo katika nchi
husika na duniani kwa ujumla. Napenda kutoa mwito kwa wadau wote kuyapa
umuhimu mapendekezo haya.
Ninafahamu kwamba tathmini kamili ya mafanikio ya utekelezaji wa
Malengo ya Maendeleo ya Milenia imepangwa kufanyika Septemba mwaka
2013. Hata hivyo tayari tunaweza kusema kuwa Malengo haya yameleta
mabadiliko chanya katika maisha ya watu wa kawaida sehemu nyingi
duniani, hususan barani Afrika. Ni dhahiri kuwa jamii nyingi
zimenufaika na utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia sio kwa
kufanyiwa hisani bali kwa wao wenyewe kuwa na mikakati maalum ya kupiga
hatua madhubuti za kujiletea maendeleo stahimilivu na yaliyolenga kuleta
usawa baina ya watu.
Mkutano wa Rio + 20
Ni jambo la kutia moyo kwamba maendeleo shirikishi na yenye kuleta
usawa ni baadhi ya masuala muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano wa Rio
+20 uliomalizika hivi karibuni. Suala hili litachukua nafasi kubwa pia
katika kuandaa mfumo wa maendeleo unaotarajiwa baada ya mwaka 2015,
mwaka uliokusudiwa kufikia malengo ya maendeleo ya milenia.
Nilipokabidhiwa jukumu la kuratibu maandilizi ya ushiriki wetu kwenye
mkutano wa Rio+20 nilitiwa moyo na nia ya dhati ya mashirika ya Umoja wa
Mataifa ya kubuni mkakati wa pamoja wa kutekeleza maazimio ya Rio+20.
Napenda kuzishukuru nchi wanachama kwa kufikia makubaliano katika
masuala mengi yaliyojadiliwa Rio licha ya changamoto nyingi zinazotokana
na mtikisiko wa uchumi duniani. Ninafurahi kwamba maazimio ya mkutano
huu yatachangia upatikanaji wa maendeleo stahimilivu, shirikishi na
yenye kuleta usawa na hususan kuhakikisha kunakuwa na mustakabali mzuri
kwa wanawake na wasichana.
Uwezeshaji wa wanawake na usawa wa kijinsia
Tukirejea kwenye suala hili, hata baada ya Mkutano wa Rio + 20
tutawajibika kuendelea na juhudi za uwezeshaji wa wanawake na kuleta
usawa wa kijinsia. Wakati wa utumishi wangu Umoja wa Mataifa tumefanya
bidii kubwa na kutumia muda mwingi kushughulikia suala hii. Tumetumia
hadhi na ushawishi wa ofisi yetu kupaza sauti za wanawake na wasichana
na kukuza ushiriki wao katika jamii. Tumeendesha kampeni za kupiga vita
ukatili kwa wanawake na wasichana. Tumezihimiza mamlaka katika ngazi za
kitaifa na kimataifa kutunga sera na sheria zinazozingatia haki za
wanawake na usawa wa kijinsia, na tumetaka wapewe fursa kushika nafasi
za uongozi katika jamii. Ndiyo maana kwa upande wetu hatukuweka koleo
chini hadi pale tulipokamilisha uanzishwaji wa idara inayojulikana kwa
kifupi kama “UN Women” mnamo Julai 2010. Hii ni idara ya Umoja wa
Mataifa iliyoundwa kwa madhumuni ya kuongoza masuala ya wanawake na
usawa wa kijinsia kwa umakini na ufanisi zaidi kuliko hapo awali.
Tumefanya jitihada hizi kwa kuamini kuwa hakuna uamuzi wowote ule, uwe
mdogo au mkubwa, unaofanywa na Umoja wa Mataifa bila ya kuzingatia
maendeleo na ustawi wa wanawake na wasichana.
Huduma ya Pamoja
Kwa upande mwingine ninapenda kuwapongeza kwa dhati wenzangu wote
waliomo katika utumishi wa Umoja wa Mataifa,wake kwa waume,walioutumia
ujuzi na weledi wao wote kuchangia maendeleo ya nchi na jamii
tunazozihudumia. Natoa shukrani za pekee kwa wale wote waliopo kwenye
ofisi na vituo vya Umoja wa Mataifa nje ya Makao Makuu na ambao
wanafanya kazi katika mazingira magumu na yenye changamo nyingi. Hao
wote wanadhihirisha umuhimu wa kuwapo kwa Shirika hili kama chombo cha
kuhimiza maendeleo katika ngazi zote za kitaifa, kikanda na kimataifa.
Katika kutekeleza dhana ya “Huduma ya Pamoja” (Delivering as One)
Waratibu Wakaazi wa Umoja wa Mataifa wamekuwa na mchango muhimu
sana.Uratibu wao umeongeza ubora na wepesi wa utoaji huduma kwa nchi
wanamowakilisha Shirika. Hatuna budi kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa
katika kufanikisha dhana ya “Huduma ya Pamoja”. Ni dhahiri kwamba
uwezo wa nchi mwanachama kumiliki mchakato wa maendeleo yake unakuwa
imara zaidi pale ambapo kuna mtiririko mzuri wa huduma za Umoja wa
Mataifa na fursa za kukuza ushirikiano endelevu na wadau wengine wa
maendeleo. Wakati uamuzi rasmi kuhusu maendeleo ya dhana hii ukisubiri
kukamilika kwa majadiliano ya nchi wanachama, ninaamini kwa dhati kuwa
utaratibu wa kutoa “Huduma ya Pamoja” kupitia mpango mmoja uliokubaliwa
na wote ni mwelekeo sahihi na wenye tija.
Nchini mwetu Tanzania, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa
yakifanya kazi kwa ushirikiano wa karibu sana toka mwaka 2011 kupitia
mpango mmoja uitwao “Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kusaidia Maendeleo”
(United Nations Development Plan – UNDAP). Mpango huu unakwenda sambamba
na mwaka wa fedha wa Serikali yaani Julai 1 hadi Juni 30 na kwa mantiki
hiyo kuuwezesha kuzingatia vipaumbele vya Serikali. Kupitia mpango huu
Umoja wa Mataifa umejiwekea utaratibu wa kujipima na kujitathmini ambao
unatoa fursa kwa hatua za haraka kuchukuliwa inapobidi. Utaratibu huu
unapatikana kwenye tovuti. Kwa upande wa uendeshaji, mfumo huu wa
utendaji kazi kwa pamoja umetuwezesha kutekeleza majukumu mengi kwa
kutumia raslimali chache ambapo“ziada” iliyopatikana imeelekezwa kwenye
shughuli nyingine za maendeleo.
Afya ya Jamii
Katika eneo la afya, ambamo wanawake na watoto ndiyo wanaathirika
zaidi, hatua muhimu zinachukuliwa kupunguza vifo na kuhakikisha kwamba
kila mwanamke na kila mtoto anakingwa na maradhi, hususan kuzuia
maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Tukiwa Nairobi Aprili mwaka 2011, Katibu Mkuu Ban Ki-moon, Michel
Sidibe, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia UKIMWI (UNAIDS) pamoja nami tulishuhudia mfano hai wa
jitihada za Umoja wa Mataifa. Tulipata fursa ya kukutana na mwanamke
aliyeathirika na virusi ambaye alijaaliwa kupata mapacha watatu
waliozaliwa bila ya maambukizi. Nikiwa mjumbe wa Kamisheni ya Umoja wa
Mataifa iliyoshughulikia taarifa na uwajibikaji katika masuala ya afya
ya mama na mtoto (Commission on Information and Accountability on
Women’s and Children’s Health) ambayo iliendeshwa kwa umahiri na Rais
Kikwete wa Tanzania na Waziri Mkuu Harper wa Canada, nina imani kwamba
jumuiya ya kimataifa hivi sasa imepata mfumo madhubuti utakaohakikisha
kwamba kunakuwa na ufuatiliaji, usimamizi na uwajibikaji kuhusu afya ya
mama na mtoto. Hakuna shaka kwamba mfumo huu utafikia hatua ya
utekelezwaji siku za hivi karibuni.
Hali kadhalika, kazi nzuri imekuwa ikifanywa na Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Shirika la Mpango wa Uzazi Duniani (UNFPA), Babatunde
Osotimehin, na Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani
(WHO) ya kuboresha afya ya mama na mtoto. Matokeo ya jitihada za
wenzangu hawayalikuwa chachu ya utekelezaji wa majukumu ya Naibu Katibu
Mkuu katika nyanja zote za maendeleo. Ama kwa hakika matunda ya kazi zao
yanaimarisha imani yangu kuwa Umoja wa Mataifa ni Shirika lenye umuhimu
mkubwa; na kwamba mchango wetu, japo mdogo, unasaidia sana katika
kufikia malengo ya maendeleo ya milenia. Nilijawa na imani kama hiyo
nikiwa katika ziara nyingine za kikazi. Kwa mfano nikiwa Montevideo,
Uruguay, Novemba 2011, pamoja na wenzangu Michelle Bachelet, Helen Clark
na Alicia Barcena, tulisimama kidete kuunga mkono kampeni ya kitaifa
ya kupiga vita vitendo vya ukatili kwa wanawake.
Nilipozuru Haiti mwezi Aprili2010, miezi michache baada ya tetemeko
ambalo lilikuwa kubwa kuliko yote yaliyowahi kutokea nchini humo kwa
kipindi cha takriban karne moja, nilikutana na watu ambao walikuwa
wameathirika vibaya sana: waliopoteza familia nzima, waliopata ulemavu
wa maisha, waliopoteza mali zao zote! Lakini bado watu hawa walikuwa na
nyuso za matumaini wakitarajia mchango wa Umoja wa Mataifa na wa wadau
wengine wa jumuiya ya kimataifa. Mnamo Novemba 2010 tulizuru Laos,
ambako Umoja wa Mataifa unashirikiana kwa karibu na Serikali na wadau
wengine wengi katika utoaji wa misaada muhimu ya maendeleo ikiwa ni
pamoja na kuisaidia Laos kupambana na janga la mabaki ya mabomu ya
“cluster munitions”.
Hii ni mifano michache tu inayojibu hoja za wakosoaji wa Umoja wa
Mataifa.Ujumbe wangu kwao ni huu: wanyonge na wenye kutaabika sehemu
zote duniani ni mashuhuda na watetezi wakubwa wa Umoja wa Mataifa. Kwa
wanyonge na wahitaji walio wengi Shirika hili ni nguzo ya kutumainiwa
katika jitihada zao za kila siku za kujiletea maisha yenye utu na
heshima.
Mageuzi katika menejimenti na usimamizi wa mabadiliko
Ukweli huu haumaanishi kuwa Umoja wa Mataifa hauna kasoro au
upungufu. La hasha! Ndiyo maana wakati wa utumishi wangu tulijielekeza
kikamilifu kwenye kuboresha masuala ya utawala, uendeshaji na namna
tunavyofanya kazi. Ni wazi kwamba hivi sasa Umoja wa Mataifa umebadilika
kutoka chombo cha huduma za mikutano na kuwa mtendaji mwenye majukumu
muhimu nje ya kumbi za mikutano. Kwa ushirikiano na msaada maridhawa wa
wafanyakazi wenzangu, tulijikita katika kuhamasisha mabadiliko ya
kiutendaji katika Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na kujenga desturi
ya uwajibikaji, uadilifu na kufanya kazi kwa tija zaidi huku tukitumia
rasilmali chache.
Ilitubidi pia kuweka mifumo thabiti ya kusimamia mabadiliko
yaliyokuwa yakijitokeza. Katika kufanya hivyo tulitambua wazi kwamba
hakukuwa na njia ya mkato wala njia mbadala ya kuliimarisha Shirika letu
na kulifanya liwe la kisasa zaidi katika kutekeleza majukumu
yake.Tulihakikisha kwamba utendaji kazi wetu unakwenda sambamba na
changamoto zilizopo, lakini pia tulizingatia ufinyu wa bajeti, misimamo
tofauti na wakati mwingine inayaokinzana ya nchi wanachama wa Umoja wa
Mataifa. Katika hali hii ilitulazimu kuwa wabunifu zaidi ili kuleta
muafaka baina ya nchi wanachama na kuhakikisha kwamba raslimali chache
zilizopo zinatoa tija kubwa zaidi.
Wafanyakazi ndiyo rasilmali kubwa kupita zote. Hivyo kila
tulipoendelea na jitihada za kuboresha Shirika ilitubidi kuwekeza
vilivyo kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kwa kuwapatia fursa za
mafunzo na msingi imara wa maendeleo yao kazini. Ni jambo lililo dhahiri
kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanatekeleza majukumu yao katika
mazingira hatarishi na yenye kubadilika mara kwa mara. Tunafahamu, tena
kwa uchungu mkubwa, kuwa Bendera ya Umoja wa Mataifa - “bendera ya
bluu” – hivi sasa si kinga tena. Haituhakikishii usalama kwani wengi
wa watumishi wetu mahiri wamekuwa wahanga wa matukio ya kikatili ya
ugaidi. Nilishuhudia tukio la aina hii huko Abuja, Nigeria, ambako
watumishi wenzetu walipoteza maisha kutokana na shambulio la kigaidi la
tarehe 26 Agosti 2011. Na mara nyingi wenzetu wanapotangulia mbele ya
haki, wapendwa wao wanaachwa katika hali ngumu ya maisha. Ni faraja
kubwa kwangu kuwa miongoni mwa masuala ambayo tuliyasimamia kabla ya
kumaliza utumishi wangu ni kuanzisha mchakato wa kubaini namna bora ya
kuwasaidia wahanga wa majanga hayo pamoja na familia zao.
Utawala wa sheria
Mojawapo ya majukumu ya Umoja wa Mataifa ni kukuza sera zinazolenga
kulinda haki za binadamu na kuendeleza utawala wa sheria katika ngazi
za kitaifa na kimataifa. Leo hii, nchi nyingi zimelipa kipaumbele suala
la kuimarisha utawala wa sheria, hususan kufuatia umuhimu wake katika
ajenda za ujenzi wa amani (peace-building) na maendeleo stahimilivu. Kwa
mantiki hiyo, nilifurahi nilipopata fursa ya kusimamia ujenzi wa mfumo
madhubuti wa sera na mwongozo wa utekelezaji wa shughuli za utawala wa
sheria nikishirikiana na nchi wanachama. Kwa upande wao nchi wanachama
zimepanga kufanya mkutano wa ngazi ya juu wakati wa kikao cha Baraza Kuu
la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba 2012. Nia kubwa ni kuendeleza
jitihada katika suala hili ili kukuza heshima ya watu wote duniani na
kujenga amani kati ya mataifa.
Hitimisho
Japokuwa muda wangu wa utumishi katika Umoja wa Mataifa umefikia
tamati, naamini hakuna tamati katika utekelezaji wa malengo, misingi na
maadili ya Umoja wa Mataifa. Ili mradi bado kuna umaskini duniani na
mahitaji ya chakula; bado kuna changamoto ya kutunza utu na heshima ya
binadamu na haja ya kuimarisha amani duniani basi hakika nitaendelea
kuunga mkono jitihada, misingi na malengo ya Umoja wa Mataifa popote
pale nitakapokuwa. Kwani ni dhahiri kwamba njia bora ya kukabiliana na
changamoto kubwa zilizo mbele yetu ni kujenga ubia na ushirikiano wa
karibu baina ya serikali, asasi za kiraia, wafanyabiashara, mashirika ya
hisani, taasisi za kitaaluma na watu binafsi.
Aidha, ninaaamini kuwa vijana, kizazi ambacho kina kila sababu ya
kuwa na kiu ya kuishi kwenye dunia yenye utu, usawa, haki na amani,
watauchukulia Umoja wa Mataifa kuwa mbia wa kuaminika katika kujenga
mustakabali wao.
Asha-Rose Migiro
No comments:
Post a Comment