BBB

advertisement

tangaza sherehe

ADVERTISEMENT

Monday, July 2, 2012

Dr Ulimboka aanza matibabu Afrika Kusini ...


 



MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka amewasili Afrika ya Kusini kuanza kupatiwa matibabu. Dk Ulimboka alisafirishwa juzi kwa ndege ya kukodi ya Shirika la Ndege la Afrika ya Kusini kwenda nchini humo, baada ya hali yake  kubadilika ghafla Alhamisi wiki iliyopita.

Jopo la madaktari lililokuwa likimhudumia, Dk Ulimboka lilitoa taarifa kuwa figo zake zimeshindwa kufanya kazi na juhudi zao kusafisha damu yake kutokutoa matokeo mazuri, hivyo kushauri apelekwe nje ya nchi kwa matibabu zaidi.
Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitage alilieleza Mwananchi jana, kuwa Dk Ulimboka alifika salama Afrika ya Kusini na kuwa kwa sasa anaendelea na matibabu.

“Habari nilizopata kutoka Afrika Kusini zinaeleza kuwa amefika salama jana (juzi) na anaendelea vizuri baada ya kupata huduma zinazohitajika,”alisema.

Dk Chitage ambaye hakuwa tayari kutaja ni hospitali gani anatibiwa, alisisitiza kuwa huduma alizozipata nchini humo zimenza kumsaidia.

Hata hivyo, habari zaidi zilizopatikana jana zilieleza kuwa Dk Ulimboka wenzake wawamekataa kutaja hospitali hiyo kwa sababu za kiusalama, na kwamba hali yake ilikuwa bado haijabadilika sana.
“Hakuna mabadiliko yoyote, walifika salama jana (juzi) na kwa kuwa anatibiwa katika hospitali ya kulipia, huduma zimeanza jana (juzi) ileile,” alisema daktari mmoja ambaye yupo karibu na Dk Ulimboka.

Mgomo
Katika hatua nyingine, Dk Chitage alisema madaktari wanaendelea na mgomo nchi nzima, licha ya vitisho vinavyoendelea kutolewa na Serikali.

“Kuhusu mgomo upo palepale, sisi tunaendelea hadi madai ya msingi tuliyotoa likiwamo la uboreshwaji wa huduma za afya pamoja na sitahili zetu yatakaposikilizwa na Serikali,” alisema Dk Chitage.

Dk Chitage alisema, madaktari kote nchini wanatarajia kukutana kujadili mambo mbalimbali kati ya leo na kesho na kutoa taarifa kwa umma kueleza matokeo yake.

Dk Ulimboka alitekwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Jumatano, akapigwa, na kujeruhiwa vibaya kisha kutupwa katika Msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Mkataba hospitali binafsi
Serikali ipo katika mchakato wa kuingia mkataba na hospitali binafsi nchini kote kuhudumia wagonjwa ambao wanakosa matibabu kutokana na mgomo wa madaktari unaoendelea nchi nzima.

Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema, Serikali imechukua hatua hiyo ili ziweze kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa.

Alisema kwa upande wa huduma za wajawazito na watoto, zitaendelea kutolewa bure katika hospitali za Serikali na binafsi.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk Gunini Kamba alisema tayari wameshaingia mkataba na Hospitali ya TMJ kutoa huduma ya matibabu katika kipindi cha mgomo uliopo.

Dk Kamba alisema huduma zitakazotolewa ni za magonjwa yote na kwamba wagonjwa watachangia kiasi kidogo cha fedha kama walivyokuwa wakichangia katika hospitali za Serikali.
Alisema wagonjwa walioandikiwa kupimwa kipimo cha CT-Scanr na X-Ray watachangia kiasi kidogo cha fedha  kama walivyokuwa wakichangia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Tayabali Jafferji alisema wamekubaliana na Serikali kutoa huduma ya matibabu ambapo mgonjwa atatoa gharama ndogo ya matibabu.

KCMC
Athari za kuondolewa kwa madaktari zaidi ya 80 katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, zinatarajiwa kuanza kuonekana leo huku hospitali hiyo ikifunga kliniki zote za wagonjwa hospitalini hapo.
Taarifa zinadai mbali na kutimuliwa kwa madaktari hao 80, baadhi ya madaktari wanaosomea ubingwa (resident doctors) zaidi ya 50 nao wamelimwa barua kutokana na kujihusisha na mgomo huo.
“Jana (juzi) jioni wanaosomea ubingwa nao walipewa barua warudi kwa Provost (mkuu wa chuo) wa chuo kikuu cha utabibu kilichomo chini ya Chuo Kikuu cha Tumaini,” kilidokeza chanzo chetu.
 Tayari Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Martin Shao amewasihi madaktari katika hospitali hiyo kuweka mbele masilahi ya wagonjwa.
Wakati huohuo, uongozi wa Hospitali ya Serikali ya Mkoa Kilimanjaro ya Mawenzi umeamua kurudisha huduma za upasuaji katika chumba cha zamani ambacho kilifungwa Desemba 27, 2010 na wataalamu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kutokana na kukosa sifa, hivyo kuifanya hospitali hiyo kutokuwa na huduma ya upasuaji.

Mtikila atoa tuhuma
Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amemtaka Rais Jakaya Kikwete kujiuzulu nafasi yake hiyo kutokana na watu wa Idara ya Usalama wa Taifa kutajwa katika tukio la kumpiga na kumjeruhi Dk Ulimboka.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam jana, Mtikila alidai kuna ushahidi wa kutosha wa watu wa idara hiyo kuhusika na alidai kuwa, baadhi yao wamejibainisha wenyewe, na mwingine aliyetambuliwa na Dk Ulimboka mwenyewe.
Alisema Rais Kikwete anapaswa kujiondoa katika nafasi hiyo vinginevyo ahakikishe watendaji wa idara hiyo ambao wanatuhumiwa kuhusika na kipigo na mateso dhidi ya Dk Ulimboka wanatiwa mbaroni badala ya kuunda tume kuchunguza suala hilo.
Kuhusu mmoja wa maofisa wa Jeshi la Polisi kupigwa na watu wenye hasira siku Dk Ulimboka alipofikishwa katika Taasisi ya Mifupa (Moi), alisema askari huyo akiwa chooni kwa kutumia ‘radio call’, alisikika akiwaeleza wenzake kuwa Dk Ulimboka hajafa hali ambayo inaonyesha kuwa kulikuwa na mpango unaotekelezwa na jeshi hilo.

Tangazo Moi
Uongozi wa Taasisi ya Mifupa (Moi) umebandika tangazo linalowataka madaktari wote wanaotaka kuendelea na kazi kujisajili, na mwisho usajili huo ikiwa ni leo.
Tangazo hilo lilitolewa baada ya kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa Moi na kilichokaa Juni 29 na kutoa siku tatu za mwisho wa wiki kwa madaktari wote kujisajili kwa Mkurugenzi wa Tiba.

Katika hatua nyingine hali katika Hospitali za Rufaa za jijini Dar es Salaam ,Amana na Temeke na Mwananyamala huduma ziliendelea kwa kusuasua kutokana na mgomo unaoendelea.
Arusha
Uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mt Meru umelazimika kuitisha kikao cha pamoja na madaktari wa hospitali hiyo kwa lengo la kuwasihi waachane na mgomo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kikao hicho kiliitishwa na Mganga Mkuu Mfawidhi, Dk Eliringia Mlay, siku moja tu baada ya Dk Ulimboka kutekwa na kisha kujeruhiwa na watu wasiojulikana.
Katika kikao hicho madaktari hao wakizungumza kwa jazba, walitishia kugoma na kubainisha ya kwamba kamwe hawawezi kuwa na ari ya kufanya kazi, ihali mwenzao kaumizwa, na hivyo kuonyesha hofu ya usalama wa maisha yao.

Dk,Mlay alipoulizwa na gazeti hili alikiri uongozi wa hospitali hiyo kuitisha kikao hicho na kubainisha ya kwamba, lengo lake lilikuwa ni kuwasihi wasigome ili kuokoa hali za maisha za wagonjwa hospitalini hapo.

Imeandaliwa na Pamela Chilongola, Joseph Zablon, Geofrey Nyang’oro, Aidan Mhando, Dar; Daniel Mjema, Moshi na Moses Mashalla, Arusha.Chanzo:gazeti la mwananchi

No comments:

Post a Comment

SHARE

TOA MAONI YAKO KUHUSU POST HII

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...