Askari wa DRC wakimbilia Uganda
Askari wa Kongo wamekimbilia na
kuingia nchini Uganda kufuatia mapigano na waasi, wakazi wa mji wa mpaka
wa Bunagana wameiambia BBC.
Wenyeji Bunagana wamesema kuwa askari wengi walikuwa wamevuka mpaka, ambapo walipokonywa silaha na jeshi la Uganda .
Inaamikia kuwa waasi wemeudhibiti mji huo kwa upande wa Kongo ambao pia upo upande wa Uganda.
Waasi wa Bosco Ntaganda walibeba silaha na kuanza mapambano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwezi Aprili.
Waasi hao ni wale waliojiondoa katika jeshi
baada ya shinikizo kuongezeka kwa serikali kumkamata Jenerali Ntaganda,
ambaye ni mshitakiwa wa uhalifu wa kivita anayesakwa na Mahakama ya
Kimataifa ya Jinai ya ICC.
Vyanzo vya habari kutoka Idara ya Usalama
vimemwambia mwandishi wa BBC Ignatius Bahizi nchini Uganda kwamba waasi
wa M23 wanadhibiti 15km wakizidi kushika kasi kuelekea mpaka wa kusini
mwa mbuga maarufu ya wanyama ya Virunga "Virunga National Park" eneo
lenye aina ya sokwe wanaishi milimani.
Wakazi wa Bunagana wanasema askari wa Kongo wamekuwa wakielekea mji wa Kisoro, ambao ni kilometa 80 kutoka mpakani.
Msemaji wa M23 Vianney Kazarama ameliambia
shirika la habari AFP kwamba waasi wameushikilia mji huo kwa upande wa
Kongo mapema siku ya Ijumaa habari ambazo pia zimethibitishwa na wakazi
wa upande wa mji huo sehemu ya Uganda .
"Waasi hao wameudhibiti mji mzima ambapo watu
wote na askari wa Kongo wapo Uganda." Chanzo cha polisi katika eneo hilo
limeiambia AFP.
Karibu watu wapatao 200,000 wameyakimbia makazi
yao baada ya mapigano ya hivi karibuni nchini Kongo, ambapo pia
inasadikiwa watu 20,000 wamevuka mpaka kuingia Uganda na Rwanda.
Umoja wa Mataifa hivi karibuni ulitoa ripoti
ikiituhumu nchi ya Rwanda kuwaunga mkono Waasi wa Jenerali Ntaganda
ambao wengi ni Watutsi ambalo ndilo kabila la uongozi wengi wa Rwanda.
Hata hivyo nchi ya Rwanda ilikanusha madai hayo kwa nguvu zote.
No comments:
Post a Comment