Mwanariadha wa Kenya matatani
Polisi nchini Kenya
wamemchukulia hatua mwanariadha mashuhuri Ezekiel Kemboi kwa madai ya
kumdunga kisu mwanamke mmoja Jumatano usiku.
Kemboi anasifika kwa mbio za mita elfu tatu
kuruka viunzi na maji. Mwanamke anayedai kufanyiwa kitendo hicho, Anne
Njeri Otieno, anadai kuwa mwanariadha huyo alimshambulia wakati
alipokataa kuwa na uhusiano wa kimapenzi naye.
Kemboi,
aliambia polisi kuwa wakati alipokuwa anamrejesgha nyumbani mwanamke
huyo katika mji wa Eldoret, walishambuliwa na watu wlaiokuwa wamejihami
na hivyo akajeruhiwa kwenye purukushani hilo.
Kemboi mwenyewe ni afisaa wa polisi na anajiandaa kwenda mjini London kwa michezo ya Olimpiki.
Hata hivyo Kemboi aliachiliwa kwa dhamana baada
ya kulipa dola 595 za Kimarekani na kesi yake itasikilizwa tena mwezi
Septemba baada ya michezo ya Olimpiki.
"Tayari niko katika kikosi cha wanariadha
watakaowakilisha Kenya kwenye michezo ya Olimpiki. Ninaomba mahakama
kunipa nafasi niweze kushiriki " alinukuliwa akisema Kemboi mbele ya
mahakama.
Mwandishi wa BBC mjini Eldoret Wanyama Chebusiri
anasema kuwa Kemboi alichukua muda wa saa saba katika kituo cha polisi
alipokuwa anahojiwa.
Kituo hicho cha polisi pia kilijaa watu waliokuwa wanataka kumuona Kemboi alipofika kwa mashtaka.
Hapo awali, Bi Otieno, ambaye anaendelea kupata
nafuu hospitalini, aliambia waandishi wa habari kwamba alikuwa kwenye
mkahawa mmoja na Kemboi wakati alipokubali kumpeleka nyumbani usiku
ulipoingia.
Mwaka 2004 Kemboi aliyeshinda dhahabu kwenye
mbio za elfu tatu aliambia polisi kuwa alivamiwa na wezi alipokuwa nje
ya gari lake na kumtaka awape pesa na kisha kumshambulia.
Alisema alichukua hatua hiyo ili kujilinda dhidi ya kuvamiwa na katika purukushani hiyo Bi Otieno akajeruhiwa.
No comments:
Post a Comment