DIDIER DROGBA
Katika siku ya kwanza la msimu wa ligi ya
Uingereza mwaka wa 2009/2010, jambo ambalo kamwe halingetarajiwa
lilikuwa linatendeka, mabingwa Chelsea walikuwa waneelekea kushindwa na
klabu ya Hull City, lakini ni mabao mawili kutoka kwa Didier Drogba
yalionyakulia timu hiyo ushindi.
Na hiyo ndio iliokuwa ishara ya kuwa,
mshambuliaji huyu mwenye umri wa miaka 32 kutoka Ivory Coast bado
alikuwa na mengi ya kuonyesha.
Tangu Januari mwaka wa 2010, Drogba amekuwa
akimiminia mabao kwa klabu na nchi yake. Amefungia Chelsea mabao 37
katika mechi 40 na kuiwezesha timu hiyo kushinda ligi ya Uingereza mara
mbili mfululizo akiwa ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye
ligi hiyo.
Kama nahodha wa timu ya taifa ya Ivory Coast
katika michuano ya Klabu Bingwa barani Africa na Kombe la dunia mwaka wa
2010, Drogba alikuwa mchezaji aliyetoa matumaini zaidi licha ya kuwa
timu yake ilishindwa kutamba kwenye mechi zake.
Kinyume na mawazo ya wengi, Drogba amenukuliwa
akisema kuwa yeye hana tamaa ya kufunga mabao. Tangu msimu huu uanze
amekuwa akiwasaidia wenzake akiwemo Salomon Kalou, Florent Malouda na
Mshambuliaji mwenzake Nicholas Anelka kutikisa wavu wa wapinzani wao na
mabao.
Drogba ni mmoja wa washambuliaji hatari kwenye
ulingo wa kambumbu sasa hivi. Hisia zake kali kuhusu mpira wakati
mwengine humsababisha kuwatolea wenzake hasira lakini licha ya hilo,
hakuna tashwishi kuwa Drogba ndiye anayetamba uwanjani wakati wowote.
Didier Drogba ndiye anafaa zaidi
Kura yangu ipo kwa Drogba kwa kuwa mchezo wake
umekuwa thabiti, na amekuwa akifunga mabao ambayo ni muhimu kwa klabu na
taifa lake.
Kama mshambuliaji amedhihirisha kuwa hajakuwa
akifunga mabao tuu bali pia amekuwa akiwaandalia wachezaji wenzake
nafasi nyingi tuu za kufunga. Hebu waulize Salomon Kalou, Florent
Malouda na Nicholas Anelka kwa nini imekuwa rahisi kufunga mabao wakati
wanapocheza kwenye upande mmoja naye.
Hakuna mchezaji wa mpira barani Afrika amekuwa
na mwaka mzuri kama mshambuliaji huyu kutoka Ivory Coast. Aliuanza kwa
mikiki na amemaliza akiwa bado yupo juu.
Mabao yake 37 katika mechi 40 yaliwezesha timu
yake ya Chelsea kushinda ligi ya Uingereza mara mbili mfululizo naye
akawa ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi kwenye ligi hiyo.
Timu ya taifa ya Ivory Coast haikufanya vyema
nchini Angola kwenye michuano ya klabu bingwa barani Afrika, lakini
umahiri wa Drogba ulijitokeza katika mechi za timu yake hadi pale
walipong'olewa katika roba fainali za michuano hiyo.
Awali kulikuwa na hofu ikiwa atashiriki kwenye
mechi za Kombe la Dunia pale alipovunjika mkono mwezi Juni tarehe 5,
lakini ukakamavu wake ulijitokeza kwenye mechi zote za kundi lao huko
Afrika kusini.
Ivory Coast walikuwa kwenye kundi lenye timu
zenye uzoefu mkubwa, lakini bila shaka Drogba aliaacha sifa kwa bao lake
alilofunga kwa ustadi kutumia kichwa ingawa timu yake ilifungwa mabao
tatu kwa moja na Brazil.
Mpende au umchukie, kunatofauti kubwa kati ya
mshambuliaji na anayefunga mabao, lakini bila shaka utapendezwa zaidi
kuwa na anayefunga mabao kwenye timu yako kuliko anayesifika tuu kwa
kuandaa mabao.
Ni kipofu tuu atakaye mnyima Didier Drogba,
nafasi ya kushinda tuzo hili la mchezaji bora wa soka wa BBC kwa mwaka
wa pili mfululizo.