Saturday, August 11, 2012

Dude abanwa, alipa deni


SIKU moja baada ya kuvamiwa na wezi nyumbani kwake, Jeti Lumo, Temeke, jijini Dar na kukombwa vitu kibao, staa wa sinema za Bongo, Kulwa Kikumba ‘Dude’ amemrejeshea fedha zake mwimba Injili, Felix Ilomo baada ya kumbana sana.
Wiki iliyopita, Ilomo alisema anajiandaa kumpandisha Dude kizimbani endapo angeendelea kumzungusha na fedha zake kiasi cha shilingi milioni nne (4,000,000) alizompa kwa ajili ya kumsaidia maandalizi ya kushuti video ya wimbo wa Kwa Neema Yako Yesu.
Ilomo alidai kuwa alimkabidhi fedha hizo Dude tangu mwanzoni mwa mwaka huu lakini kila akiulizia siku ya kushuti video hiyo, msanii huyo alikuwa akimzungusha na kumwambia mtu wa kufanya kazi hiyo alisafiri nje ya Jiji la Dar.
Paparazi wetu alipompata Dude kwa njia ya simu alikiri kurejesha fedha hizo lakini akasema si kwa sababu ya kutishiwa kupandishwa kortini bali alilipa kwa hiari yake kwa vile yeye alikuwa muunganisha mipango na si mtendaji, hivyo hata kama angeacha asingeathirika chochote.
“Nimeona nimpe tu fedha zake ndugu yangu huyu mtumishi wa Mungu lakini ukweli ni kwamba fedha nilimkabidhi George ambaye ndiye alikuwa amfanyie video yake ila kwa sababu ameshindwa kumvumilia acha nimlipe mimi halafu George akirudi Dar atanirejeshea,” alisema Dude.
Usiku wa kuamkia Jumatano ya Agosti 8, 2012, Dude aliingiliwa na majambazi nyumbani kwake ambako waliiba samani kadhaa.
Kwa mujibu wa Dude mwenyewe, yeye alikuwa ‘lokesheni’ kwa ajili ya kurekodi filamu ila familia yake, yaani mkewe (Eva) na watoto walikuwepo.
Alisema wezi hao walipuliza dawa inayosadikiwa ni ya kumfanya mtu alale fofofo na ndipo walipopata nafasi ya kuvunja milango na kukomba vitu.
Alisema ameshafungua kesi kwenye Kituo cha Polisi cha Jeti Lumo ambapo msako mkali wa kuwanasa wezi hao unaendelea.

No comments:

Post a Comment

SHARE

TOA MAONI YAKO KUHUSU POST HII

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...