Timu changa na mpya kwenye
mashindano ya soka Afrika Mashariki na Kati Azam ya Tanzania imefanikiwa
kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano ya Cecafa.
Azam, iliyomaliza ligi ya Tanzania msimu
uliopita ikiwa nafasi ya pili, ilisajiliwa Ligi Kuu ya Vodacom mwaka
2007 na inamilikiwa na tajiri mwenye viwanda nchini Tanzania, Salim
Bakhresa.
Azam
ilifuzu kutoka Kundi C baada ya kutoka suluhu ya kutofungana na Tusker
ya Kenya. Mafunzo nayo ilifuzu kutoka Kundi hilo, huku Tusker wakitupwa
nje ya mashindano.
Timu nyingine ambazo zimeingia robo fainali ni bingwa mtetezi Yanga ya Tanzania na mahasimu wao Simba.
Vita Club kutoka DR Congo, URA kutoka Uganda,
APR ya Rwanda na Atletico ya Burundi ndizo timu nyingine zilizofanikiwa
kutinga nane bora.
Mechi za robo fainali zitachezwa Jumatatu na
Jumanne. Mechi za Jumatatu zitakuwa kati ya APR na URA na Yanga dhidi ya
Mafunzo. Simba watacheza na Azam na Vita Club watacheza na Atletico
Jumanne.
Mbali na Tusker, timu nyingine zilizoaga
mashindano baada ya mzunguko wa makundi ni Al Salaam Wau ya Sudan Kusini
na Ports ya Djibouti.
Mshindi wa mashindano atazawadiwa dola 30,000 huku mshindi wa pili na tatu wakipata dola 20,000 and 10,000.
Fedha zitatolewa na Rais wa Rwanda Paul Kagame, ambaye mashindano haya yamepewa jina lake.

No comments:
Post a Comment