BBB

advertisement

tangaza sherehe

ADVERTISEMENT

Wednesday, June 27, 2012

USIKU WA WEMA HAIJATOKEA













JUNI 23, mwaka huu ndani ya Hoteli ya Hyyat Kilimanjaro Kempinski iliyopo Posta jijini Dar, staa wa filamu, Wema Isaac Sepetu alizindua filamu yake ya Super Star na kufanya mambo makubwa ambapo wadau walisema haijawahi kutokea Bongo, Risasi Mchanganyiko lilishuhudia.
Usiku huo ambao Wema aliutumia kuzindua filamu hiyo uliwakutanisha mastaa kibao na watu wengine mashuhuri ambapo vituko vya hapa na pale vilitawala.
Hakukuwa na kiingilio katika uzinduzi huo lakini ilikuwa ni lazima mtu apewe kadi maalum au atumiwe ujumbe wa simu wa mualiko.
Kwa upande wa burudani, wasanii kutoka nyumba ya vipaji, THT, msanii wa filamu anayefanya muziki wa mduara, Zuwena Mohammed ‘Shilole’ na mwanadada wa Bongo Fleva, Sarah Kaisi ‘Shaa’ walitumbuiza katika uzinduzi huo.
REDI KAPETI ILIKUWEPO
Kama kawa, zulia jekundu liliwekwa kwa ajili ya wageni waalikwa kupita na kupiga picha za mapozi tofauti.
KULA, KUNYWA BURE
Ndani ya ukumbi huo, vinywaji na vyakula vilikuwa bure kwa kila aliyetinga kushuhudia uzinduzi wa filamu hiyo inayodaiwa kuwa na matukio ya kweli yanayomhusu staa huyo aliyetwaa taji la urembo la Tanzania mwaka 2006.
VITUKO
Mastaa kama vile, Vincent Kigosi ‘Ray’ Halima Yahya ‘Davina’ na Jacob Steven ‘JB’ waliwaongoza wengine kukata nyonga zao ili kupamba usiku huo wa Wema.
Aidha, mwanamitindo Jacqueline Patrick, Belina Mgeni na mastaa wengine waliokuwa wamevalia viatu virefu walishindwa kujiachia navyo hivyo kulazimika kuvivua ili wawe huru kucheza muziki wa Kwaito.
Katika kuweka vionjo, mastaa hao walishindana kucheza huku wengine wakichuana katika kutunza ambapo Ray na Steven Mangere ‘Steve Nyerere’ walichukua nafasi ya upedeshee.
UZINDUZI RASMI WA FILAMU
Huku watu wakiendelea kula bata, mshereheshaji wa hafla hiyo ambaye ni Mtangazaji wa Redio Times ya jijini Dar, Khadija Shaibu ‘Dida’ aliwaomba wageni waalikwa kuingia katika ukumbi mwingine kwa ajili ya kuzindua filamu hiyo.
“Wageni waalikwa nawaomba muingie katika ukumbini wa Level Eight kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa filamu yetu,” alisikika Dida akisema.
MINONG’ONO KUHUSU OMOTOLA YATAWALA
Wakati muda ‘ukitaradadi’, minong’ono ilianza kutanda ukumbini hapo kwamba Wema kawapiga wadau ‘changa la macho’ juu ya ujio wa staa kutoka Nigeria, Omotola Jalade.
“Unafanya mchezo nini kumleta staa kutoka Nigeria, aliweza marehemu Kanumba tu tena kwa kusaidiwa na Steps siyo Wema,” alisikika akibwatuka staa mmoja wa tasnia ya filamu Bongo.
OMOTOLA ATUA USIKU WA MANANE
Wakati kila aliyekuwa katika sherehe hiyo akiamini Omotola asingeweza kufika Bongo, mishale ya saa 9:00 usiku MC alitangaza kuwa muda wa kwenda kumpokea mgeni huyo umewadia hivyo msafara wa kwenda Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere ulianza.
Ilipotimu saa 9: 15 usiku, Omotola alitua na kumfanya Wema ‘kupiga bao’ kwa kudhihirisha kwamba hakuwa akitania aliposema anamleta staa huyo.
Hata hivyo, Omotola alipotinga ukumbini alikuta baadhi ya wadau wa filamu walishaondoka kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda sana.
KALI ZAIDI
Mbali na kukodi ukumbi wa hoteli hiyo, Wema pia alikuwa amemkodia Omotola vyumba viwili, kimoja kwa ajili ya kulala na kingine kwa ajili ya kubadilishia nguo na kupambwa (kufanyiwa make-up).
Hali kadhalika, Wema naye alikuwa na vyumba viwili katika hoteli hiyo vilivyokuwa na matumizi kama ya Omotola.
GIRAFFE HOTELI
Kama vile haitoshi, uzinduzi wa filamu hiyo uliendelea usiku wa siku ya pili Juni 23, mwaka huu katika Hoteli ya Giraffe iliyopo Mbezi Beach jijini Dar ambapo Omotola alikuwa mgeni rasmi.
Huko nako Wema na Omotola walimiliki vyumba viwiliviwili kwa ajili ya kujipamba na kulala.
Katika ukumbi wa hoteli hiyo, Bendi ya Sky Night ilitumbuiza na Mtangazaji Benny Kinyaiya alikuwa MC ambapo watu wa kawaida walitakiwa kulipa shilingi 30,000 kushuhudia uzinduzi huo.
Kabla ya uzinduzi, mabibi wanaoshiriki Shindano la Bibi Bomba linaloendeshwa na Kituo cha Clouds TV walipita katika redi kapeti na kuonesha manjonjo yao.
Baada ya hapo, MC alimkaribisha Wema ambaye alisema machache kisha akamkaribisha mgeni wake kunena chochote kabla ya kuzindua rasmi filamu hiyo na kuwaacha watu wakiiangalia.
Baada ya tukio hilo, wadau wengine wakiwemo mastaa wa Bongo walionesha vituko vingine kwa kugombania kupiga picha na Omotola ambapo kutokana na vurugu, watu walitakiwa kupanga mstari ili kutimiza zoezi hilo.
Wakati shughuli hiyo ilipofikia kikomo, Wema na baadhi ya watu mashuhuri walienda katika ufukwe wa Ngalawa uliopo karibu na hoteli hiyo ambako waliendelea kujiachia.
Kwa tukio hili, Wema amevunja rekodi ya kutengeneza filamu kwa gharama kubwa lakini pia amevunja rekodi kwa kufanya pati ya nguvu.
MASWALI MAGUMU
Pamoja na Wema kufanikisha uzinduzi huo, wadau wamekuwa wakijiuliza staa huyo amepata wapi fedha za kufanyia mambo yote hayo.
WEMA ANASEMAJE?
Risasi Mchanganyiko, lilimuuliza Wema gharama alizotumia kukodi ukumbi huo ambapo hakuwa tayari kuweka bayana zaidi ya kutaja gharama za maandalizi ya filamu hiyo ambayo ni shilingi milioni 68.

1 comment:

SHARE

TOA MAONI YAKO KUHUSU POST HII

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...